Watoto milioni 20 hawapati chanjo ya magonjwa hatar
16 Julai 2019Ripoti ya mwaka kuhusu utoaji wa chanjo ulimwenguni iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF imeeleza kuwa viwango vya chanjo vinashuka hasa kwenye nchi masikini duniani au maeneo yenye mizozo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa chanjo ni moja ya nyenzo muhimu zaidi katika kuzuia mlipuko wa magonjwa na kuiweka dunia kuwa sehemu salama.
Maskini wako hatarini zaidi
Ghebreyesus amebainisha kuwa mara nyingi walio hatarini ni maskini, walioathiriwa na mizozo au waliolazimika kuyakimbia makaazi yao pamoja na wanaodharaulika.
Ripoti hiyo ya WHO na UNICEF imegundua kuwa tangu mwaka 2010, upatikanaji wa dozi tatu za chanjo ya dondakoo, pepopunda na kifaduro na dozi moja ya chanjo ya surua zimefikia kiasi cha asilimia 86.
UNICEF imesema ingawa asilimia hiyo ni ya juu, bado sio ya kuridhisha, na kwamba asilimia 95 ya chanjo inahitajika ulimwenguni kote ili kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.
Mwaka 2018, idadi ya wagonjwa wa surua duniani kote iliongezeka mara mbili zaidi na kufikia 350,000, ikilinganishwa na mwaka 2017. Kwa mwaka 2018, Ukraine iliongoza orodha ya nchi kadhaa kwa kuwa na visa vya juu vya surua, ingawa nchi hiyo imefanikiwa kutoa chanjo kwa zaidi ya asilimia 90 ya watoto wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietha Fore, anasema kuwa surua ni kiashiria tosha ya kwamba wana kazi zaidi ya kufanya ili kuzuia magonjwa. Fore anasema mlipuko wa ugonjwa huo unaeleza kuwa jamii hazipati chanjo na wanatakiwa kuongeza juhudi kuhakikisha kila mtoto anapatiwa chanjo.
Nchi 16 hazijatoa chanjo kwa watoto
Karibu nusu ya watoto ambao hawajapatiwa chanjo wanatoka katika nchi 16 duniani, ikiwemo Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Ethiopia na Haiti. Nchi nyingine ni Iraq, Mali, Niger, Pakistan, Somalia, Sudan Kusini, Syria na Yemen.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa iwapo watoto hao wataugua, watakuwa katika hatari ya kukabiliwa na madhara mabaya zaidi ya kiafya na hawatoweza kupata matibabu na huduma wanayohitaji.
Kwa kushirikiana na Muungano wa mashirika ya kutoa chanjo-Gavi, WHO na UNICEF zinazisaidia nchi mbalimbali kuimarisha mifumo yao ya kutoa chanjo na kuzuia milipuko ya magonjwa, ikiwemo kwa kuwachanja watoto wote, kuendesha kampeni za dharura na kutoa mafunzo na vifaa kwa wafanyakazi wa afya, ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha huduma ya afya ya msingi.