Uhaba wa maji shuleni na vyoo ni changamoto kwa wanafunzi
27 Agosti 2018Karibu watoto milioni 900 wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya msingi vya usafi wanapokuwa mashuleni, hali inayosababisha afya zao kuwa hatarini na kusababisha wengine kukosa shule. Viongozi wa dunia wametoa ahadi za kutoa maji safi na vifaa vya usafi kwa ajili ya wote na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kufikia mwaka 2030 chini ya malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Uhaba wa maji salama na vifa vya usafi kunaweza kusababisha ukosefu wa maji mwilini, maradhi na pia vifo. Lakini watoto wengi wanalazimika kuhatarisha afya zao ili kwenda shule, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani, ikiwa ni ripoti ya kwanza kumulika huduma zinazotolewa mashuleni.
Ripoti hiyo imegundua kwamba karibu theluthi moja ya shule za msingi na sekondari hazikuwa na huduma ya maji safi ya kunywa na ya uhakika, na kuathiri karibu watoto milioni 570. Karibu asilimia 20 ya shule hazina maji safi ya kunywa kabisa. Zaidi ya theluthi moja ya shule zinakosa vyoo, na kuathiri zaidi ya watoto milioni 620. Shule moja kati ya tano za shule ya msingi na moja kati ya nane za sekondari zinachukuliwa kuwa hazina usafi.
Karibu nusu ya shule hizo hazikuwa na vifaa muhimu vya kuosha mikono ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuwasaidia kuepuka maambukizi na magonjwa. Ripoti hiyo imebainisha kwamba watoto milioni 900 waliathiriwa na hali hiyo. Nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara, Asia Kusini na Mashariki zilikuwa na miundombinu mibovu. Wasichana wanaobalehe hususan ndio mara nyingi hulazimika kukosa masomo wanapokuwa katika hedhi kama hakuna miundombinu bora ya usafi.
Zaidi ya theluthi moja ya wasichana huko Asia Kusini wanakosa masomo wanapokuwa katika hedhi, kwasababu mara nyingi hawapati huduma ya vyoo, taulo za kike, taarifa hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mapema mwaka jana na shrika la WaterAid na UNICEF. Benki ya dunia mwaka jana ilionya kwamba nchi zilitakiwa kuongeza matumizi yake hadi kufikia dola bilioni 150 kwa mwaka ili kuwezesha upatikanaji wa maji safi na huduma ya vyoo.
Hata hivyo wataalamu wana wasiwasi kwamba hali hiyo inaweza kuimarika kwa haraka endapo tu viongozi watalichukulia suala la maji, vyoo na usafi kama kipaumbele na kwamba utashi wa kisiasa utawezesha utoaji wa huduma bora.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Thomson Reuters Foundation
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman