Watoto Syria wanaishi katika mazingira magumu
9 Machi 2016Ripoti hiyo iliyokusanywa kutokana na mahojiano yaliyofanyiwa wasyria wanaoishi katika maeneo yaliyozingirwa, wakiwemo watoto wa miaka 10 hadi 16, wazazi, na wataalamu kama madaktari na walimu, inakadiria zaidi ya watoto laki mbili na nusu wameathiriwa na mapigano na kunyimwa haki zao za msingi, katika maeneo yaliyozingirwa.
Sonia Khush, Mkurugenzi wa shirika la Save the Children eneo la Syria, amesema watoto wa Syria huenda wakakumbana na madhara ya muda mrefu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kwa takriban miaka mitano.
Sonia amesema kwa sasa jamii wanaoishi katika maeneo yaliyozingirwa wameomba msaada wa kuanza mpango wa kilimo ili wajitegemee wenyewe kuliko kuendelea kutegemea misaada ya Kimataifa.
Ripoti ya shirika hilo la misaada inaendelea kusema, kuna changamoto kubwa ya mashirika ya misaada kufikia maeneo yaliyozingirwa na kwamba asilimia 1 ya vyakula vya misaada kutoka Umoja wa Mataifa iliwafikia wasyria katika maeneo hayo mwaka wa 2015.
Kulingana na mfanyakazi wa misaada ya kiutu kutoka Syria aliyezungumza na waandishi habari ambaye hakutaka kujulikana, watu katika maeneo hayo hawawezi kufikia mahitaji muhimu kama vile mikate.
Mfanyakazi huyo anayeishi dakika kumi na tano kutoka maeneo yaliyozingirwa anasema ukosefu wa chakula umewalazimu watu kutafuta mbinu mpya ya kuishi kwa kutumia nyasi kupikia supu, huku wakati wa baridi watoto wakionekana kukimbilia majengo yaliyoharibiwa kwa mabomu kuokota mbao kutumia kama kuni kuwashia moto wa kupikia na kujikinga kwa baridi.
Hata hivyo mfanyakazi huo wa misaada ya kiutu amepongeza juhudi za baadhi ya wasyria kutafuta njia za kufikisha misaada katika maeneo hayo na kujaribu kutafuta elimu kwa watoto hao. "Kama raia wa Syria ni muhimu kwangu kushiriki katika shughuli hii ya utoaji wa misaada ya kiutu, naamini juhudi za kuijenga nchi yangu zimeanza na hii inatokana na namna unavyomuelimisha mtoto," alisema mfanyakazi huyo.
Njia pekee ya kuwaokoa watoto ni kumaliza mapigano na kuachiwa maeneo yaliyozingirwa.
Michael Klosson, kaimu rais anayeshughulikia masuala ya sera na misaada katika shirika hilo la save the children amesema njia pekee ya kuwaokoa watoto katika eneo hilo ni kutozingirwa kwa maeneo na kuhakikisha misaada inawafikia walengwa.
Mapigano yaliyodumu takriban miaka mitano nchini Syria yamesababisha mauaji ya robo milioni na kusababisha wengine takriban nusu ya idadi ya watu nchini Syria kupoteza makaazi yao.
Kwengineko mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria staffan de Mistura amesema mazungumzo ya amani kati ya maafisa wa serikali ya Syria na wawakilishi wa upande wa upinzani yanatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu wiki ijayo.
Duru hiyo mpya ya mazungumzo ilitarajiwa kufanyika tangu Urusi na Marekani walipoongoza makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa februari 27 ambapo machafuko yameshuhudiwa kupungua kwa kiasi kikubwa.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP
Mhariri: Josephat Charo