Watoto wa Gaza wapambana na hisia mbaya za vita
29 Desemba 2014Muntaseer Bakr, mvulana wa miaka 11, alinusurika kufa kwa makombora ya Israel kwenye majira ya mwaka huu ya kiangazi, lakini mdogo wake wa kiume na binami zake watatu hawakupona.
Miezi mitano sasa na akiwa amewahi kufanya jaribio la kujiua, mvulana huyu wa Kipalestina bado anaendelea kuandamwa na kumbukumbu kali na simanzi za vita hivyo.
Bado anakumbuka vile ambavyo wiki moja tu baada ya mashambulizi ya siku 50 ya Israel yaliyoanza Julai na kumalizika Agosti, makombora mawili yalipoangukia kwenye ufukwe mjini Gaza ambako yeye na wenzake walikuwa wakicheza mpira. Wanne kati yao, wote wakiwa na umri wa kati ya miaka 9 na 11, waliuawa.
Naye, kama ilivyo kwa maelfu ya watoto wengine, sasa anakabiliana na vita vya ndani ya nafsi yake mwenyewe ili kuzishinda kumbukumbu mbaya na madhara ya kisaikolojia yaliyosababishwa na vita.
Gaza ilipoteza na ingali inapoteza
Mapigano yaliyoendelea kwa wiki sita baada ya mashambulizi hayo ya ufukweni, yaliwauwa Wapalestina 2,200 na kuwajeruhi zaidi ya 10,000. Kwenye eneo hilo ambalo wengine wanaliita gereza la wazi na eneo linalokaliwa na watu wengi zaidi duniani, zaidi ya nusu ya Wapalestina milioni 1 na laki nane ni watoto walio chini ya umri wa miaka 14.
Hapana shaka, wao ndio hasa wanaolipia gharama ya vita wanavyopigwa wazazi wao. Zaidi ya watoto 500 waliuawa - thuluthi moja wakiwa chini ya umri wa miaka 12. Watoto ni robo ya waliojeruhiwa.
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linasema maelfu ya watoto wana uhitaji mkubwa wa msaada wa kisaikolojia ili waweze kukabiliana na madhara ya muda mrefu ya kiakili yaliyosababishwa na vita hivyo.
Anaishi 'dunia nyengine'
Baba yake Muntaseer, Ahed Bakr, mwenye umri wa miaka 55 anasema tangu tukio la ufukweni ambapo nduguye na binami zake wanne waliuawa, mwanawe huyo amekuwa akitibiwa kwenye kituo cha wagonjwa wa akili.
"Endapo ahadi yake ya kukutana na daktari imechelewa au akachelewa kupata dawa, hata kwa dakika kumi tu, basi ni tabu kuweza kumdhibiti," anasema baba huyo.
Bakr, ambaye alimpoteza mwanawe mwenye umri wa miaka tisa, Zakaria, naye pia anaonekana kuwa na wasiwasi kama wa mwanawe, Muntaseer, ambaye haishi kula kucha zake.
Anasema mzazi huo kuwa miongoni mwa mambo anayoyafanya mvulana wake huyo ni pamoja na kupiga makelele, kuvunja kila kitu, kujigonga kichwa ukutani na hata ameshawahi kujaribu kujirusha kutoka kwenye paa la nyumba yao.
Kuna siku, anasema Bakr, walimkuta Muntaseer akijaribu kuwatundika binami zake wengine. Kwa ujumla, tangu kuuawa kwa ndugu zake mbele ya macho yake wakati wakicheza mpira, Muntaseer anaonekana kuishi dunia nyengine kabisa. Hataki kwenda skuli.
Mzigo wa taswira mbaya
"Vipi kama atajaribu kuwauwa wanafunzi wenziwe darasani?" Anauliza baba yake. Lakini mwenyewe Muntaseer anasema hataki tena kusoma kwa kuwa hapo kabla alikuwa akienda skuli na nduguye Zakaria, ambaye akimsaidia kumtajia herufi za jina lake na kuliandika, lakini sasa ameshakufa.
Ghafla anapiga makelele: "Sitaki kufanya chochote. Nataka tu nipate bunduki ya Kalashnikov niwauwe wote kulipiza kisasi cha Zakaria na binami zangu."
Kisha mvulana huyo ananyamaza kimya, kabla ya kuelezea namna anavyowaota usingizini ndugu zake hao, ambao anasema hujiona amewashika mikono yao, huku akiapa kutorejea tena ufukweni kucheza mpira, kwani huko ndiko walikouawa.
Mtaalamu wa masuala ya afya, Dokta Samir Zaqqut, anasema watoto wa Gaza wameumizwa mno kihisia kuweza kuishi maisha ya kawaida, kwani taswira walizobebeshwa na vita ni mbaya sana na haiwezekani kuzifuta.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga