1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa Sudan Kusini wanaishi kwa kula majani

11 Juni 2026

Shirika la kimataifa la hisani kwa watoto, Save the Children limesema familia na watoto katika jimbo la Jongeli nchini Sudan Kusini wanaishi kwa kula majani na maua huku kiwango cha njaa kikikaribia kuwa janga.

Sudan Kusini l Vita l Njaa
Wananchi wa Sudan Kusini wanakabiliwa na njaaPicha: Maura Ajak/AP/picture alliance

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika la Save the Children inaeleza kuwa baadhi ya maeneo katika jimbo lililokumbwa na vita la Jonglei, familia na watoto wanaishi kwa kutegemea mimea hiyo iliyokusanywa kutoka kwenye mabwawa na mbegu zilizohifadhiwa kwa ajili ya kupandwa, huku akina mama wakitembea umbali mrefu kwenda kwenye maeneo yenye mafuriko kutafuta chochote kinachofaa kuliwa na watoto wao.

Tabisa Ajer, mwenye umri wa 31, alinukuliwa na Save the Children akisema kuwa mwaka huu ni hatari zaidi kuliko miaka mingine iliyopita. Tabisa, mfanyakazi wa afya katika Hospitali ya Bor huko Jonglei, amebainisha kuwa ukosefu wa usalama unaathiri kilimo cha mazao ya chakula.

Mamilioni wanakabiliwa na njaa Sudan Kusini 

Takwimu za hivi karibuni kutoka Shirika la Kutathmini Usalama wa Upatikanaji wa Chakula Duniani, IPC, zinaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 7.8 nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na njaa kali na maeneo kadhaa ya nchi hiyo yako katika ukingo wa kukumbwa na baa la njaa.

Kulingana na IPC, takribani watu milioni 2.2 wenye chini ya umri wa miaka mitano, wanahitaji matibabu ya utapiamlo, ikiwemo watoto wapatao 700,000 wanaougua utapiamlo mkali.

Umoja wa Mataifa umesema mabilioni ya dola yameporwa serikaliniPicha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Deng, ambaye ni mkimbizi na mmoja wa akina mama ambao wanawapeleka watoto wao kutibiwa utapiamlo katika hospitali ya Save the Children iliyoko kwenye kambi ya wakimbizi ya Bor, anasema mtoto wake amekuwa akisumbuliwa utapiamlo.

''Mtoto wangu aliumwa sana. Nikampeleka hospitali na akapata nafuu ndani ya siku chache. Lakini niliporudi tu nyumbani, hali ikabadilika na kuwa mbaya tena,'' alisisitiza Deng.

Mashambulizi yasababisha Save the Children kusitisha baadhi ya shughuli

Shirika la Save the Children limefafanua kuwa njaa kali imewalazimisha maelfu ya watoto kuacha shule, huku wengi wakilazimika kuingia katika ajira za utotoni na ndoa za mapema. Hata hivyo, shirika hilo la misaada limesitisha baadhi ya miradi yake, baada ya mashambulizi ya makundi yenye silaha, na uharibifu wa vifaa vyake.

Chris Nyamandi, Mkurugenzi wa Save the Children nchini Sudan Kusini, anasema kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kunaendelea kuwaathiri kwa kiasi kikubwa wale walio katika hatari zaidi kwenye moja ya majimbo yasiyo na usalama duniani. Nyamandi ameongeza kusema kuwa suluhisho la kuepukana na njaa kali ni la kisiasa, na kwamba hali hiyo inaweza kuzuiwa, kabla watoto wengi zaidi hawajateseka.

Ukosefu wa usalama unaathiri kilimo cha mazao ya chakulaPicha: Luis Tato/AFP

Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan mnamo mwaka 2011, lakini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na bado inakabiliwa na umasikini uliokithiri, ufisadi na ukosefu wa usalama.

Jimbo la Jonglei, limekuwa eneo kuu la ghasia, ambako vikosi vya serikali vinavyomtii Rais Salva Kiir vinapambana na wanamgambo wanaoshirikiana na mpinzani wake wa muda mrefu, Riek Machar.

Raia wanapaswa kulindwa

Save the Children imezitolea wito pande zinazohasimiana nchini Sudan Kusini kuweka kipaumbele katika kuwalinda raia, kuheshimu sheria ya kimataifa za binaadamu, na kuhakikisha huduma za kijamii zinafika salama katika jamii zote ambazo tayari zimeathiriwa na vita.

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yamesema kuwa wanasiasa wasomi wamepora mabilioni ya dola kutoka serikalini, hali iliyowaacha wananchi wa Sudan Kusini kuwa moja ya watu maskini zaidi duniani, bila ya kuwa na huduma au msaada wowote.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW