1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 10 wachinjwa Msumbiji

Sekione Kitojo
30 Mei 2018

Polisi ya Msumbiji imesema watu 10 wamechinjwa na kundi la watu wenye silaha katika jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Cabo Delgado, eneo ambalo mashambulizi ya Waislamu wenye itikadi kali yaliwahi kuripotiwa.

Karte Mosambik Gorongosa National Park ENG

Vijana  wawili  wa  kiume  ni  miongoni  mwa  wale  waliokatwa shingo  zao  siku  ya  Jumapili, msemaji  wa  polisi  ya  Msumbiji Inacio Dina  aliwaambia  waandishi  habari , na  kuongeza  kwamba polisi  sasa  wameanzisha  msako  kuwatafuta  waliohusika. Dina alithibitisha  kwamba  kuna  watu  kutoka  nje  ya  nchi  pamoja  na raia  wa  Msumbiji   katika  kundi  hilo  la  washambuliaji.

"Hili  ni  kundi  ambalo  kwa  kiasi  kikubwa  ni  dhaifu. Kile tulichokishuhudia  ni  kukata  tamaa  kwa  kiasi  kikubwa  kwa  kundi hili  kwa  kujaribu  baadhi  ya  viongozi wa  kundi  hili  kufanya  uhalifu huu  wa  kinyama."

David Machimbuko kiongozi wa jimbo la Cabo DelgadoPicha: DW/N. Issufo

Hakuna  mtu  ambaye  amekwisha  kamatwa  hadi  sasa  kwa  mujibu wa  msemaji  huyo  wa  polisi  Inacio Dina. Hata  hivyo  hakutaka kukihusisha  kitendo  hicho  na  kundi  ambalo  liliwauwa  zaidi  ya watu  20  katika  jimbo  la  Cabo  Delgado  mwezi  Oktoba, ama iwapo  kuna  uhusiano  na  kundi  la  Waislamu  wenye  itikadi  kali. Ripoti  kutoka  katika  eneo  hilo  zinazungumzia  kwamba washambuliaji  wana mahusano  na  makundi  ya  itikadi  kali  ya Kiislamu.

Msumbiji  ambayo  kwa  kiasi  kikubwa  ina  waumini  wengi  wa Kikristo , katika  pwani  ya  kusini  mashariki  mwa   bara  la  Afrika hakujakuwa  na  makundi  ya  waislamu  wenye  itikadi  kali  hapo kabla.

al-Shabaab Msumbiji

Mapema  mwaka  huu , taarifa  moja  katika  tovuti  ya  kituo  cha kukusanya  mawazo  kilicho  na  makao  yake  makuu  nchini Marekani cha  Kituo  cha  Afrika  cha  mitaala  ya  mikakati kimesema  shambulio  la  Oktoba , liliwapata  "wachunguzi  wa mapambano ya wapiganaji  wa kimataifa wa jihadi  kwa  mshangao."

Hata  hivyo , taarifa  hiyo  ilisema , kundi "linalofahamika  ndani ya nchi  hiyo  kama  al-Shabaab  na  Swahili  Sunnah yanaonekana kuwavutia  watu  wapya  wa  kulitumikia  kundi  hilo"  nchini Msumbuji.

Bila  ya  kutaja  kundi  hilo  la  washambuliaji  kwa  jina, msemaji  wa polisi  Dina  aliapa kwamba  watawasaka  na  kuwakamata  watu wote  waliohusika  na  kitendo  hicho na  kuwafikisha  mahakamani.

Ramani ya Msumbiji

"Kile  kinachofanyika  ni  kuwasaka  wale  waliohusika  na kuwafikisha  kizuwizini  na  kuwawajibisha  kwa  njia  ya  sheria kama wengi  wengine  ambao  tayari  wamefikishwa  mbele  ya  sheria  na kuwajibishwa."

Jimbo  la  Cabo  Delgado  limeshuhudia  mashambulizi  kadhaa yaliyofanywa  na  wanaoshukiwa   kuwa  Waislamu  wenye  itikadi kali  tangu  mwezi  Oktoba mwaka  jana. Mmoja kati  ya  wahanga katika  shambulio  la  hivi  karibuni  alikuwa  kiongozi  wa  kijiji  cha Monjane, mkaazi  wa  eneo  hilo , bila  ya  kutaja  jina  lake kwa  hofu ya  kulipiziwa  kisasi.

Walimshambulia  kiongozi  huyo  kwa  kuwa  alikuwa  anatoa  taarifa kwa  polisi  juu  ya  maeneo  ambayo  kundi  la  al-Shabaab  liko katika  msitu, aliliambia  shirika  la  habari  la  afp , akimaanisha kundi  lenye  silaha  linaloaminika  kuhusika  na  shambulio  la  mwezi Oktoba  katika  kituo  cha  polisi  na  kituo  cha  upekuzi  cha  kijeshi katika  mji  wa  Mocimboa da Praia.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo