1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 10 wauwawa kwenye milipuko Nairobi, Kenya

Josephat Nyiro Charo16 Mei 2014

Watu wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa katika milipuko miwili kwenye eneo la shuguli nyingi la soko, Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ametoa risala za rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hizo.

Anschlag in Nairobi
Picha: Reuters

Kituo cha kitaifa cha operesheni za majanga kimesema mlipuko wa kwanza umetokea ndani ya matatu ya abiria 14 na wa pili ukatokea ndani ya soko la mitumba la Gikombaa, linalopatikana mashariki mwa eneo la kibiashara la jiji la Nairobi. Simon Itahe, msemaji katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, amesema maiti nane zimepelekwa hospitalini hapo na zaidi ya watu 70 wamelazwa kwa ajili ya matibabu, wengi wao wakiwa katika hali mbaya. "Wengi wa majeruhi wanavuja damu nyingi. Tunahitji damu," akasema msemaji huyo, wakati alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Taarifa za vyombo vya habari vya Kenya zimesema mabomu yalivurumishwa ndani ya matatu na duka moja katika soko la Gikomba. Picha zimeonyesha matatu nyekundu ikiwa na madirisha ambayo vioo vyake vimelipuliwa na eneo linalozunguka mahala palipotokea milipuko hiyo likiwa limejaa kifusi na takataka nyingine.

Mkuu wa jshi la polisi katika kaunti ya Nairobi, Benson Kibue, amesema mabomu hayo yalirushwa wakati mmoja huku akijaribu kuwatuliza raia waliokusanyika na kuwahakikishia kwamba polisi wameidhibiti hali ya mambo.

Muda mfupi kabla milipuko ya leo kutokea ubalozi wa Marekani jijini Nairobi ulitoa tahadhari mpya kwa Wamarekani ukiwaonya juu ya kitisho kinachozidi kuendelea kuwepo nchini Kenya ambako ubalozi huo ulishambuliwa mwaka 1998.

Maafisa wa polisi wakipig doria eneo la GikombaPicha: Reuters

Rais Kenyatta aapa kupambana na ugaidi

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye ameanza mkutano na vyombo vya habari dakika chache baada ya mashambulizi hayo, ametoa risala za rambirambi kwa jamaa za wahanga lakini akapuuzilia mbali tahadhari zilizotolewa na Marekani na Uingereza, akisema ugaidi ni tatizo linalojulikana kila mahala, hata katika miji ya New York na Boston nchini Marekani.

"Sitaki kutaja mtu yeyote hasa. Matukio kama hayo yaliyofanywa jana na watu uliowataja yanaimarisha ari na azma ya magaidi badala ya kutusaidia kuvishinda vita dhidi ya ugaidi," akasema Kenyatta.

"Sisi tunaendelea kukabiliana na ugaidi katika taifa letu na mambo ya ugaidi hayahusu Kenya peke yake, ni nchi nyingi mpaka nyingize zinazowaondoa raia wake hapa wamepigwa na magaidi na wananchi wao wameuwawa. Hivi ni vita ambavyo nataka tukabiliane navyo dunia nzima. Langu ni kuwaomba Wakenya tuendelee kuwa imara, tuendelee kuhakikisha tumejikinga, na pia tuhakikishe tumepambana na ugaidi katika taifa letu la Kenya. Marafiki zetu ambao wangetusaidia twawashukuru na tutaendelea kusaidiana nao."

Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/AA

Kenyatta aidha amesema Kenya itaweka kamera 2,000 mjini Nairobi na Mombasa kusaidia kupambana na ugaidi.

Rais Kenyatta akosoa tahadhari ya usafiri

Mashambulizi hayo yametokea wakati kukiwa na wimbi la mashambulizi ya mabomu na majaribio ya kufanya mashambulizi ya mabomu katika mji mkuu Nairobi na mji wa bandari wa Mombasa katika pwani ya kenya. Yanakuja siku chache baada ya mataifa kadhaa kutangaza tahadhari kwa raia wao kutosafiri kwenda Kenya.

Siku ya Alhamisi na leo Ijumaa mamia ya watalii wa Uingereza walikuwa wakiondolewa kutoka hoteli zilizopo karibu na mji wa Mombasa kwa sababu ya tahadhari hiyo ya usafiri. Mapema mwezi huu watu watatu waliuwawa na wengine 86 kujeruhiwa katika milipuko miwili iliyotokea Mombasa.

Kenyatta amesema anafahamu onyo la Uingereza na uamuzi wa kuwaondoa raia wake waliokuwa wakitalii pwani ya Kenya. "Na la mwisho ni kusema kama Wakenya pia wale ambao wana uwezo wa kuchukua likizo, badala ya kwenda pia nchi hizo waendelee kusaidia sekta yetu ya utalii na ndio tuweze kuendelea wakati pia serikali inaendelea na mipango yake ya kupanua soko la utalii katika nchi nyingine. Mimi naendelea tu kuhimiza usalama ni wetu sisi sote kama Wakenya tushirikiane."

Mashambulizi yanaweza kutokea popote

Wanajeshi wa Marekani wenye silaha wamekuwa wakipiga doria katika viwanja vya ubalozi wa nchi hiyo jijini Nairobi. "Tunafahamu kutokana na uzoefu iwe ni Yemen ambako balozi zimeshambuliwa au Benghazi Libya ambako ubalozi wetu mdogo na balozi wetu alishambuliwa, kitu chochote chenye nembo ya nchi ya kigeni kinakabiliwa na hatari ya kulengwa katika shambulizi," amesema Scott Gration, balozi wa zamani wa Marekani nchini Kenya.

Polisi akijaribu kuwadhibiti wafanyabiashara GikombaPicha: Reuters

Gration, meja jenerali msataafu wa jeshi la Marekani anayeendesha kampuni ya kutoa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya teknolojia na uwekezaji mjini Nairobi, amesema balozi hulengwa kila mara iwe kumetolewa onyo ama la. "Huwa kama smaku kwa watu wenye malengo ya kiitikadi," akaongeza kusema Gration.

Gration amesema kampuni nyingi za utalii zina sera za bima zisisoruhusu wasafiri kuwa katika maeneo yanayokabiliwa na hatari kubwa. Amesema pwani ya Kenya ni eneo zuri la kuvutia na sana sana huwa salama. "Naamini kila mahali kuna matatizo fulani na sote tunahitaji kuwa waangalifu kuhusu wakati tunapotembea na wapi tunakotembea. Kwa hiyo sisafiri usiku, najiepushe na halaiki ya watu na nafunga milango yangu. Uwe Newark, New Jersey au Nairobi, Kenya, tunaweza kuwa wahanga wa uhalifu au ugaidi."

Mwandishi: Josephat Charo/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman