1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 wafariki kwenye maporomoko, DRC

Michael Kwena
9 Machi 2026

Watu mia moja wanahofiwa kufariki baada ya kufukiwa kwenye mgodi wa kuchimba madini ya coltan katika ajali mbaya ya hivi karibuni Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | machimbo | madini
Watu zaidi ya 100 wamefariki dunia kwenye machimbo ya coltan huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Zheng Yangzi/Xinhua News Agency/picture alliance

Maporomoko hayo ya ardhi yalitokana na mvua kubwa zilizonyesha katika mji wa Masisi ulio katika jimbo la Kivu Kaskazini. Maafisa wa idara ya uokozi wanaendelea kuwatafuta manusura na pia kuitafuta miili ya watu waliokufa.

Mvua kubwa zinaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku matokeo yake yakisababisha madhara makubwa.

Msemaji wa polisi nchini humo Robert Kasongo ameliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa kwamba, maafisa wa idara ya uokoaji wanaendelea na juhudi za kuwatafuta manusura baada ya mkasa huo ambao kwa sasa maafa yake yameongezeka.

Maporomoko hayo ya ardhi yametokea siku chache tu baada ya tukio kama hilo kutokea wiki iliyopita katika mgodi mwingine wa kuchimba madini ya koltan katika eneo hilohilo la Masisi huko Kivu Kaskazini ambako watu 200 walifariki wakiwemo watoto 70. Wizara ya madini katika taarifa yake imesema watu kadhaa pia walijeruhiwa.

Je, ni nani anayenufaika kweli na madini adimu ya Rubaya?

07:40

This browser does not support the video element.

Ni janga linalotishia uhai wa watu

Aidha,makumi ya watu pia waliripotiwa kufariki mwanzoni mwa mwezi Januari kufuatia tukio jingine la maporomoko ya udongo kwenye migodi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hali ya mazingira ya kazi kwenye migodi mingi nchini Kongo imeripotiwa kuwa ni hatarishi, licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ya madini. kwa kiwango kikubwa hakuna vifaa vya usalama kwa wachimbaji wa madini huku ajira ya watoto likichukuliwa kuwa ni jambo la kawaida.

Migogoro inayoripotiwa nchini humo pia imeripotiwa kuzidisha hali hiyo. Tangu katikati ya mwaka 2024, eneo la Masisi limekuwa likithibitiwa na waasi wa M23 ambao wanasimamia shughuli za uchimbaji katika eneo hilo na maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.

Migogoro hiyo inachochewa na rasilimali nyingi za madini kama vile koltani, dhahabu na bati. Koltani, inayotumika kutengeneza metali ya tantali, ina umuhimu mkubwa katika utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki na ni muhimu katika bidhaa kama simu za mkononi na kompyuta.

Zaidi ya wapiganaji 100 wenye silaha na wanajeshi wanaoaminika kutoka Rwanda wamekuwa kwenye mzozo wa takriban miaka 30 nchini Kongo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW