1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza

29 Februari 2024

Wizara ya afya katika ukanda wa Gaza, imesema watu 104 wameuwawa katika shambulio la anga, dhidi ya wapalestina waliokuwa wanasubiri kupokea misaada.

Mgogoro wa Gaza| Hopsitali ya Al-Aqsa
Watu zaidi ya 100 wameuwawa wakati wa kupokea msaada wa kibinaadamu Gaza.Picha: AFP/Getty Images

Msemaji wa wizara ya afya Ashraf al-Qidra  amesema watu wengine 280 wamejeruhiwa katika tukio hilo. Fares Afana, mkuu wa kitengo cha huduma za magari ya kubebea wagonjwa katika hospitali ya Kamal Adwan, amesema wataalamu wa afya waliofika katika eneo la tukio waliwakuta mamia ya watu wakiwa sakafuni na kwamba hapakuwa na magari ya kutosha ya kubebea maiti na wale waliojeruhiwa, na ilibidi wengine wapelekwe hospitalini kwa kutumia mikokoteni inayoendeshwa na punda.

Israel kwa upande wake imelielezea tukio hilo kama janga. Msemaji wa serikali ya taifa hilo Avi Hyman, amesema kile kinachojulikana kwa sasa ni kwamba madereva wa malori ya chakula walilemewa na kuyaendesha magari yao kwawapalestina waliokuwa wanasubiri misaada.

Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza

Amesema pia watu wengi wamekufa kutokana na mkanyagano na kusukumana wakati wa kupokea misaada hiyo. Avi Hyman amesema hicho ndicho anachokijua kwa sasa na hana habari yoyote ya Israel kufanya mashambulizi katika eneo la tukio.

Lakini ofisi ya rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas imelikosoa shambulizi hilo ililoliita "mauaji yaliyofanywa na jeshi la Israel" dhidi ya watu waliokuwa wakisubiri misaada katika eneo Nabulsi.

Hamas yaonya mashambulizi zaidi yatakwamisha juhudi za amani

Hamas ambalo ni kundi lililoorodheshwa kama kundi la kigaidi na Ujerumani, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine, limeonya kwamba tukio hilo huenda likasababisha kufeli kwa mazungumzo yanayonuiwa kupata ufumbuzi wa mgogoro huo, kati ya Israel na kundi hilo na huenda pia ikakwamisha juhudi za kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa mjini Gaza.

Mashambulizi hayo yamaliharibu kabisa  eneo hilo lililotengwa kwa miezi kadhaa na hata kudhibitiwa kwa misaada ya kiutu kufika huko. Makundi ya kutoa misaada yamesema imekuwa vigumu kufikisha misaada katika maeneo mengi ya Gaza, kutokana na kwamba makundi ya watu walionauhitaji wa msaada huo, kurundikana katika malori ya misaada na kufanya iwe vigumu kuganwanya misaada hiyo. Kulingana na Umoja wa Mataifa wapalestina milioni 2.3 wanakabiliwa na baa la njaa.

Haniyeh: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini pia kuendeleza mapigano

Mji wa Gaza na eneo zima la Kaskazini mwa mji huo ndio maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi ya angani, baharini na ardhini na jeshi la Israel, ikijibu mashambulio ya Hamas yaliyotokea kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7.

Huku hayo yakiarifiwa kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema mpango wa Israel wa kufanya operesheni za ardhini katika mji wa Rafah katika ukanda wa Gaza utakwenda kinyume na amri ya Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ, iliyosema siku ya jumatatu kwamba Israel inapaswa kukomesha visa vyote vinavyochukuliwa kama mauaji ya halaiki.

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

02:41

This browser does not support the video element.

ap/afp/reuters