Watu 11 wauawa katika mashambulizi Kongo
15 Februari 2021Tukio hili lilifanyika mapema asubuhi wakati wanamgambo hao waliposhambulia maghala mawili ya silaha ya Kimbembe na Kibati mjini Lubumbashi. Wanamgambo wa kundi la Bakata-Katanga wanashukiwa kuendesha shambulizi hilo.
Akiwa mjini Lumbumbashi, Waziri wa Mambo ya Ndani katika Jimbo la Haut-Katanga, Moise Panga Dibale akiwa amesema milio ya risasi ilisikika katika maeneo mengi ya Lubumbashi, wakati ambapo jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilipambana na wanamgambo hao.
''Matokeo ni kama ifuatavyo; kwa upande wa wanamgambo: watano wamekamatwa, saba wamekufa, silaha nne zimepatikana. Kwa upande wa jeshi la FARDC, wanajeshi watatu waliuawa, msichana mdogo aliuawa kisha kupigwa risasi na wake wanne wa askari walijeruhiwa. Kwa sasa hali imedhibitiwa,'' alifafanua Waziri Dibale.
Mjini Kinshasa, Waziri wa taifa anayehusika na mambo ya ndani, Gilbert Kandonge alikutana na viongozi husika na usalama ili kulijadili suala hilo. Mkutano huo ulibaini kwamba shambulizi hilo liliendeshwa na vijana wanamgambo wa kundi la Bakata-Katanga wanaofanya ghasia katika mji huo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Silaha kadhaa zapatikana
Msemaji wa polisi Kanali Pierrot Mwanamputu, akiwa mjini Kinshasa amesema vikosi vya FARDC vilifanikiwa kupata silaha 12 pamoja na risasi za vita, mapanga na kadhalika, kulikuwa pia na kamera ya kupiga picha, simu tano za mkononi, bango lililokuwa limeandikwa maneno "Jamhuri ya Katanga” na pia ramani ya jiji la Lubumbashi.
Bakata-Katanga ni kundi la wanamgambo wanapigania kujitenga kwa mkoa wa Katanga ya zamani. Djef Mbiye ni mwanaharakati wa shirika la raia mjini Lubumbashi. Anakanusha kwamba shambulizi hilo halihusiani na mvutano ulioko sasa kati ya Rais wa zamani Joseph Kabila na Rais Félix Tshisekedi:
Mwanaharakati huyo anasikitikia hali ya kuwa wanaotumiwa katika mashambulizi ya aina hiyo ni watoto wa vijiji vya Katanga ambao baadhi yao hawajui wanachokifanya, na wala wengine hata hawajawahi kufika ndani ya mji huo wenye madini.