Watu 13 wadaiwa kuuawa na kundi la RSF
4 Novemba 2024Haya ni kwa mujibu wa chanzo kimoja cha matibabu kilicholiarifu shirika la habari la AFP.
Chanzo hicho kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimesema kikosi hicho cha RSF kiliwafyetulia risasi watu hao katika mji wa Al-Hilaliya.
Jimbo la Al-Jazira nchini Sudan limekuwa kitovu cha mapigano tangu kamanda wa RSF, Abu Aqla Kaykal, alipotangaza kuliasi kundi hilo na kujiunga na upande hasimu wa jeshi la taifa.
Soma pia:Mpango wa Chakula, WFP waomba utulivu nchini Sudan ili litoe huduma zake
Kulingana na mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami, RSF ilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo ya mashariki ya jimbo la Al-Jazira kati ya Oktoba 20 na 25.
Afisa huyo amesema wanamgambo hao wanatuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki, vitendo vya unyanyasaji watu kingono, uporaji mali kwenye masoko na majumba pamoja na kuchoma moto mashamba.