Watu 14 wafariki Congo baada ya mgodi kuporomoka
3 Oktoba 2019Matangazo
Takriban watu 14 wamefariki baada ya mgodi mmoja kuporomoka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hapo jana.
Watu wengine 20 hawajulikani walipo baada ya ajali hiyo katika mgodi wa dhahabu kwenye mji wa Kampene mashariki mwa Congo. Haya ni kulingana na waziri wa masuala ya kibinadamu Steve Mbikayi.
Kwa mujibu wa mkuu wa shirika moja la kijamii Stephane Kamundala, wafanyikazi katika migodi hiyo ya dhahabu wanafanya kazi bila mashine.
Ameongeza kusema kuwa ajali hiyo inaaminika kusababishwa na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo.
Taifa hilo la Afrika ya Kati lina utajiri mkubwa wa dhahabu, shaba na almasi pamoja na madini ya kobalti na coltan ambayo inahitajika sana kwa sababu ya matumizi yake katika simu za mkononi.