Watu 146 wamekufa Indonesia
21 Februari 2005Jakarta:
Watu wasiopungua 146 wameuawa leo nchini Indonesia kutokana na mporomoko wa ardhi uliosababishwa na mvua kubwa. Mporomoko umetokea alfajiri wakati watu walikuwa wamelala na kuharibu kabisa nyumba zaidi ya 70 mjini Cimahi, karibu na Bandung, umbali wa km 200 kusini mashariki mwa Jakarta. Nyumba zote zimefunikwa kwa matope na takataka nyingine. Waokoaji kutoka jeshini, polisi na wakazi wanajitahidi na harakati zao za uokozi wakitumaini kuwaokoa wale ambao hawaonekani. Lakini juhudi zao zinakwamishwa kutokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya ardhi huenda ikaporomoka. Mporomoko wa ardhi hutokea mara kwa mara nchini Indonesia na hasa wakati wa majira ya mvua kisiwani Java. Itakumbukwa kuwa Watu 42 wamekufa magharibi mwa Sumatra mwaka wa jana wakati Basi lao lilipofunikwa na tani za udongo, vifusi na miti.