Watu 15 wafa baada ya boti kugongana
4 Februari 2026
Naibu Meya wa kisiwa hicho, Pantelis Vroulis, aliiambia televisheni ya umma, ERT, kwamba miili 15 ndiyo iliyoopolewa na yote ilikuwa ya wahamiaji.
Televisheni hiyo ilitangaza kuwa watu 25 walikuwa wamepelekwa kwenye hospitali ya kisiwa hicho, 11 wakiwa watoto wadogo na wawili wakiwa maafisa wa kikosi cha ulinzi wa pwani.
Vyombo vya habari vinasema watu kadhaa walikuwamo kwenye mashua hiyo ya wahamiaji iliyokuwa ikitokea Uturuki kuelekea Kisiwa cha Chios.
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR kiasi cha wahamiaji 1,000 wameingia kwenye visiwa vinavyotawaliwa na Ugiriki kwenye Bahari ya Aegan wakitokea Uturuki tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Sababu za ajali yatajwa
Ajali hiyo ilitokea baada ya mashua ya Walinzi wa Pwani kujaribu kuikamata boti ya wahamiaji na kuilazimisha kugeuza njia. Kulingana na taarifa ya Walinzi wa Pwani, "Nahodha wa boti hiyo ya mwendo kasi ambayo haikuwa na taa za kuiongoza na aliyewabeba abiria wa kigeni alikataa kuheshimu ishara za maonyo zilizotolewa na Walinzi wa Pwani."
Badala yake, nahodha huyo aligeuza boti hiyo na kisha kugongana na upande wa boti ya doria ya Walinzi wa Pwani," imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa "mgongano ndio ulisababisha boti hiyo kupinduka na kuzama."
Idadi kubwa ya wahamiaji bado wanazama ama kupotea baharini
Idadi kubwa ya wahamiaji huvuka Bahari ya Mediterania kila mwaka wakijaribu kuingia Ulaya. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilisema mwezi Novemba kwamba zaidi ya watu 1,700 walikufa ama kupotea mwaka 2025 kwenye njia mbalimbali zinazotumiwa na wahamiaji kwenda Ulaya katika Bahari ya Mediterania na katika Bahari ya Atlantiki pembezoni mwa pwani ya Afrika magharibi.
Na kulingana na Shirika la Wahamiaji ulimwenguni, IOM, karibu wahamiaji 33,000 wamekufa ama kupotea kwenye Bahari ya Mediterania tangu 2014.