Watu 15 wauwawa kwenye mapigano Somalia
7 Desemba 2010Mapigano mapya makali yamesababisha vifo vya kiasi ya watu 15 wengi wao raia wa kawaida katika eneo la katikati mwa Somalia. Kwa mujibu wa maafisa wa serikali na viongozi wa kitamaduni, mapigano hayo yalizuka jana jioni baada ya wapiganaji wa ukoo mmoja waliojihami kwa silaha nzito walipolishambulia eneo lililoko mbali na mji wa Galkayo, ulioko kwenye mpaka na eneo la Puntland lililojitenga na eneo la kati la Somalia. Kulingana na taarifa za shirika la habari la AFP, mpaka sasa maiti 11 zimesafirishwa hadi eneo lililo kusini mwa Galkayo.
Mapigano hayo yalikuwa kati ya ukoo wa Saad unaolimiliki eneo la Galmudug na wapiganaji wa Majerteen wanaotokea Puntland. Koo hizo mbili zimekuwa zikihasimiana kwa muda mrefu kwa sababu ya uhaba wa maji na ardhi.