1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 17 wauawa Afghanistan

Prema Martin26 Februari 2010

Hadi watu 17 wameuawa Kabul katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Taliban waliojitolea mhanga.Raia wa kigeni ni miongoni mwa wale waliouawa katika shambulio baya kabisa kupata kufanywa Kabul tangu mwaka mmoja.

An Afghan police officer looks at the body of an unidentified man lying in the rubble at the scene of an explosion at a guesthouse in Kabul, Afghanistan, Friday, Feb. 26, 2010 (AP Photo/Ahmad Massoud)
Polisi akisimama karibu na hoteli mojawapo iliyoteketezwa katika mripuko wa bomu mjini Kabul.Picha: AP

Kwa mujibu wa polisi na mashahidi, wanamgambo waliojitolea mhanga walishambulia katikati ya Kabul kwenye eneo lenye hoteli ndogo ndogo wanakoishi wafanyakazi wa Ubalozi wa India na wageni wengine. Wataliban wamedai kuwa wao ndio waliohusika na shambulio hilo mapema leo asubuhi na kuongezea kuwa lilifanywa na wanamgambo wao watano. Eneo hilo la Kabul ni maarufu pia kwa maduka yake mengi na huwavutia matajiri wa Kiafghanistan.

Maafisa wa Afghanistan wanasema, hadi watu 17 wameuawa na si chini ya 37 wengine wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, mwananchi  mmoja wa nchi hiyo ameuawa katika shambulio hilo. Wakati huo huo, Zemarai Bashari wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mtaliana vile vile ni miongoni mwa wale waliouawa. Kwa upande mwingine, Ubalozi wa India umethibitisha kuwa raia wake wapatao 6 wamejeruhiwa na kiasi ya 3 wengine hawajulikani walipo.Katika shambulio la leo, mripuko mmoja mkubwa na mingine miwili midogo iilitokea wakati Waafghanistan wakiadhimisha Maulidi-siku ya kuzaliwa Mtume Mohammad.

Kwa mujibu wa polisi, wanamgambo wawili wengine walipigwa risasi kabla ya kushambulia. Milio ya risasi ilikuwa ikisikika katika eneo hilo huku magari ya hospitali yakikimbilia kuchukua majeruhi. Eneo hilo kati kati ya mji mkuu Kabul lina ulinzi mkali na lilikua shwari tangu shambulio la Januari 18. Katika shambulio hilo Wataliban waliovamia majengo ya biashara na ofisi katikati ya Kabul walijiripua kwa mabomu na walisababisha vifo vya hadi watu 5.

Shambulio la hii leo ni baya kabisa kupata kufanywa mjini Kabul tangu majeshi ya NATO na vikosi vya Afghanistan chini ya uongozi wa Marekani kuanzisha operesheni kubwa dhidi ya ngome ya Wataliban katika Wilaya ya Helmand kusini mwa Afghanistan, ikiitwa "Operesheni Mushtarak." Kwa mujibu wa NATO, wanajeshi wake 2 wameuawa nchini Afghanistan lakini kwa sasa haikutajwa ni raia wa nchi gani. Kifo kimoja kilitokea leo hii wakati wa Operesheni ya Mushstarak na mwengine aliuawa siku ya Alkhamisi katika mripuko wa bomu lililofichwa ardhini. Mabomu hayo yaliyofukiwa chini ya ardhi na Wataliban yamesababisha vifo vya wanajeshi wengi wa kigeni nchini humo.

Kikosi cha Marekani kikiingia Marjah kusini mwa Afghanistan kama sehemu ya Operesheni Mushtarak.Picha: AP

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mwaka huu, wanajeshi 99 wameuawa Afghanistan ambako kiasi ya wanajeshi 121,000 wanapambana na Wataliban waliotimuliwa madarakani  kufuatia uvamizi wa mwaka 2001 ulioongozwa na Marekani.  "Operesheni Mushtarak" iliyoanzishwa February 13 ni sehemu ya mkakati mpya unaoazimia kumaliza vita vya miaka minane nchini Afghanistan. 

Mwandishi:P.Martin/AFPE

Mhariri:Othman,Miraji