Watu 17 wauwawa kwenye mapigano ya wanajeshi na waasi Niger
28 Juni 2008NIAMEY
Takriban watu 17 wanasemekana wameuwawa katika mapigano kati ya wanajeshi na wafuasi wa kundi la waasi la kikabila la Tuareg nchini Niger.
Maafisa wamethitisha kutokea mapigano hayo kwenye eneo la mji ulioko kaszini wa Tezirzait na wamesema kwamba waliouwawa ni waasi na hakuna hata mwanajeshi mmoja aliyeuwawa.Hata hivyo waasi hao wa kundi linalojiita la kupigania haki la Movement for Justice MNJ limesema wanajeshi 26 wa serikali wameuwawa pamoja na wapiganaji wake sabaa.
Kundi hilo linapigania kuweko maendeleo katika eneo la kabila la watuareg na pia eneo hilo lifaidike kutokana na mapato ya madini ya Uranium yanayotoka kwenye eneo hilo.Hata hivyo serikali ya Niger inapinga madai ya kundi hilo na kulitaja kuwa kundi la majambazi na wafanyibishara wa madawa ya kulevya,silaha na halina agenda ya kisiasa.Wanajeshi wamekuwa wakipambana mara kwa mara na wanachama wa kundi hilo huku serikali ikikataa kuzungumza na waasi hao hadi pale watakapoweka chini silaha.