1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiKorea Kusini

Watu 179 wafariki katika ajali ya ndege Korea Kusini

29 Desemba 2024

Watu 179 wamepoteza maisha katika ajali mbaya zaidi ya ndege katika historia ya Korea Kusini baada ya ndege ya shirika la Jeju Air kuanguka wakati ilipokuwa inatua na kuwaka moto katika uwanja wa ndege wa Muan.

Korea Kusini | Muan | Ajali ya ndege
Timu ya zima moto wakijaribu kuzima moto kwenye ndege iliyoanguka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Muan mkoa wa Jeolla Kusini, Korea Kusini.Picha: Yonhap via REUTERS

Kulingana na wizara ya uchukuzi ya Korea Kusini, ndege hiyo ya shirika la Jeju Air, chapa 7C2216, ikitokea mji mkuu wa Thailand, Bangkok, ikiwa na abiria 175 na wafanyikazi sita wa ndege, ilijaribu kutua katika uwanja huo uliopo kusini mwa nchi mapema asubuhi.

Wafanyikazi wawili wa ndege wameokolewa wakiwa hai, huku maafisa wakieleza kuwa wengine wote waliobaki huenda wamefariki.

Soma pia: Putin aiomba radhi Azerbaijan bila kukiri kuhusika na ajali ya ndege 

Ajali hiyo ya ndege katika ardhi ya Korea Kusini pia inatajwa kuwa mbaya zaidi iliyohusisha shirika la ndege la Korea Kusini katika muda wa takriban miongo mitatu, kulingana na wizara ya uchukuzi.

Ndege aina ya Boeing 737-800 yenye injini mbili ilionekana katika video zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari vya nchi hiyo ikianguka kabla ya kugonga ukuta na hatimaye kuwaka moto.

Mmoja wa manusura wa ajali ya ndege akisafirishwa hadi hospitalini huko Mokpo, Korea Kusini, Jumapili, Desemba 29, 2024.Picha: Cho Geun-young/Yonhap/AP/picture alliance

"Sehemu ya nyuma ya ndege hiyo ndiyo iliyoonekana kunusurika kidogo, ila sehemu nyingine iliyobaki haitambuliki kabisa," Mkuu wa kikosi cha zima moto cha uwanja wa ndege wa Muan Lee Jung-hyun ameuambia mkutano na waandishi wa habari.

Wafanyikazi wawili wa ndege, mwanamume na mwanamke, waliokolewa kutoka sehemu ya nyuma ya ndege hiyo iliyowaka moto. Wawili hao walikimbizwa hospitali ili kutibiwa kutokana na majeraha waliyoyapata.

Soma pia: Takriban watu 28 waokolewa wakiwa hai katika ajali ya ndege

Timu ya uchunguzi inachunguza tukio la ndege kuingia kwenye injini na hali mbaya ya hewa kama chanzo ambacho huenda kimesababisha ajali hiyo. Shirika la habari la Yonhap limenukuu mamlaka za uwanja wa ndege zikisema hatua ya "ndege kuingia kwenye injini" huenda kulisababisha hitilafu wakati ndege hiyo ilipojaribu kutua.

Mamlaka inaendelea kutafuta miili zaidi katika maeneo ya karibu ambayo huenda ilitupwa nje ya ndege hiyo.

"Maneno yangu ya mwisho"

Saa kadhaa baada ya ajali hiyo, baadhi ya familia za wahanga zilikusanyika katika eneo la mapokezi la uwanja wa ndege, wakilia na kukumbatiana huku wafanyikazi wa shirika la msalaba mwekundu wakiwapa mablanketi.

Familia hizo zimeonekana kububujikwa na machozi wakati majina ya wahanga 22 waliotambuliwa kupitia alama za vidole yalipotangazwa. Karatasi zilisambazwa kwa familia za wahanga kuandika maelezo binfasi na nambari zao mawasiliano.

Wafanyikazi wa kutoa misaada wamefika katika eneo la ajali ya ndege katika uwanja wa ndege wa Muan, kusini magharibi mwa Korea Kusini.Picha: NEWSIS via Xinhua/picture alliance

Magari ya kubeba maiti yalionekana kuwa tayari kubeba miili huku mamlaka ikieleza kwamba imetenga vyumba maalum vya kuhifadhi maiti kwa muda.

Kulingana na mashuhuda, wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa eneo kulikotokea ajali hiyo lilinuka mafuta ya ndege na damu, huku wafanyikazi waliovaa barakoa na wanajeshi wakishika doria.

Ajali hiyo ni mbaya zaidi inayohusisha shirika la ndege la Korea Kusini tangu ajali ya ndege ya shirika la Korean Air iliyotokea mjini Guam mwaka 1997, ambapo zaidi ya watu 200 walifariki.

Ripoti ya ajali ya ndege ya Ethiopia yatolewa

01:08

This browser does not support the video element.

Kulingana na wizara ya uchukuzi, ajali nyengine mbaya kuwahi kutokea katika ardhi ya Korea Kusini ni ile ya shirika la ndege la Air China iliyosababisha vifo vya watu 129 mnamo mwaka 2002.

Mnara wa kuongoza ndege ulitoa tahadhari juu ya "ndege kuingia kwenye injini" ya ndege hiyo ya Jeju Air na muda mfupi baada ya marubani kutangaza hali ya dharura, walijaribu kutua.

Soma pia: Ajali ya ndege yauwa watu 61 Brazil 

Shirika la habari la News1 limeripoti kuwa, abiria mmoja alituma ujume kwa familia yake akisema kuwa, ndege waliingia kwenye injini ya ndege iliyopata ajali. Ujumbe wa mwisho wa mtu huyo ulikuwa, "Je, niseme maneno yangu ya mwisho?"

Kulingana na wizara ya uchukuzi, kulikuwepo na abiria wawili wa Thailand na wengine wote waliosalia wanaaminika kuwa raia wa Korea Kusini.

Ndege hiyo ilitengenezwa mnamo mwaka 2009.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW