1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 18 wauawa katika siku ya umwagaji damu Myanmar

28 Februari 2021

Polisi nchini Myanmar imewafyatulia risasi waandamaji leo ikiwa ni siku mbaya kabisa ya umwagaji damu tangu maandamano yalipoanza wiki kadhaa zilizopita dhidi ya mapinduzi ya kijeshi. Watu 18 wameripotiwa kuuawa

Myanmar Yangon Putsch Proteste Polizei Verhaftung
Picha: REUTERS

Polisi waliingia mitaani mapema na kufyatua risasi katika maeneo tofauti ya mji mkubwa kabisa wa Yangon baada ya mabomu ya kushtua, ya kutoa machozi na milio ya risasi angani kushindwa kuyavunja maandamano. Wanajeshi pia waliungana na polisi.

Myanmar imekumbwa na machafuko tangu jeshi lilipochukua madaraka na kumuzuilia kiongozi wa serikali aliyechaguliwa Aung San Suu Kyi na maafisa wengine wa chama chake mnamo Februari mosi, likidai udhanganyifu katika uchaguzi wa Novemba ambao chama chake kilipata ushindi wa kishindo.

Afisa wa Umoja wa Maatifa ambaye hakutaka jina lake litambulishwe amesema ofisi hiyo imethibitisha karibu vifo vya watu watano mjini Yangon.

Polisi watuhumiwa kwa matumizi ya nguvu kupindukiaPicha: Ye Aung Thu/AFP

Mwanasiasa Kyaw Min Htke ameiambia Reuters kuwa polisi ilifyatua risasi za moto mjini Dawei kusini mwa nchi, na kuwawua watu watau, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Soma pia: Polisi Myanmar yatumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji

Gazeti la Myanmar Now limeripoti kuwa watu wawili wameuawa katika mji wa pili wa Mandalay. Vikosi vya usalama vilifyatua risasi tena na kumuuwa mwanamke mmoja, kwa mujibu wa Sai Tun, mkaazi wa Mandalay.

"Timu ya madaktari ilimuangalia na kuthibitisha kuwa alifariki dunia. Alipigwa risasi kichwan.” Alisema Sai Tun.

Polisi na msemaji wa baraza tawala la kijeshi hawakujibu simu za kuwataka wazungumzie habari hizo.

Kiongozi wa kijeshi Jenerali Min Aung Hlaing alisema wiki iliyopita kuwa mamlaka zinatumia nguvu zisizopindukia kuwakabili waandamanaji. Hata hivyo, kiasi ya waandamanaji 14 wameuawa mpaka sasa katika machafuko hayo. Jeshi linasema polisi mmoja ameuawa.

Balozi wa Myanmar katika UN Kyaw Moe Tun atimuliwaPicha: UN Geneva/dpa/picture alliance

Ukandamizaji huo unaonekana kudhihirisha dhamira ya jeshi kuonyesha mamlaka yake kutokana na upinzani unaoshuhudiwa, sio tu kutoka kwa maandamano ya mitaano, lakini pia katika utumishi wa umma, utawala wa manispaa, idara ya mahakama, sekta za elimu na afya na vyombo vya habari.

Soma pia: Jeshi la Myanmar ladai kwamba halikuipindua serikali

Taarifa ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema hatua ya vikosi vya usalama vya Myanmar ya kuongeze mvutano kwa kutumia nguvu kupindukia katika miji mbalimbali….ni ya kusitikisha na isiyokubalika.

Ubalozi wa Canada umesema umeshangazwa sana na muenendo wa ongezeko la vurugu na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.” Na Indonesia, ambayo imechukua usukani katika Jumuiya ya Mataifa ya Kusini mashariki mwa Asia – ASEAN katika juhudi za kuutatua mgogoro huo, imesema imeingiwa na wasiwasi mkubwa.

Reuters
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW