1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 18 wauawa na zaidi ya 100 wajeruhiwa Iraq

Sylvia Mwehozi
29 Oktoba 2019

Watu 18 wameuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa nchini Iraq, baada ya vikosi vya usalama kuwashambulia waandamanaji waliokaidi marufuku ya kutotembea usiku katika jimbo la Karbala. 

Irak Proteste in Kerbala
Picha: Getty Images/AFP

Shambulio hilo limetokea usiku wa kuamkia Jumanne, wakati raia wa Iraq walipomiminika mitaani kwa siku ya tano mfululizo, wakipinga ufisadi wa serikali, ukosefu wa huduma na madai mengine. Maandamano hayo ya papo kwa papo yamekabiliwa na risasi pamoja na gesi ya kutoa machozi tangu siku ya kwanza. Shambulio la Jumanne usiku lilitokea katika viwanja vya elimu mjini Karbala, kiasi ya kilometa 2 kutoka kaburi la Imam Hussein ambako waandamanaji waliweka mahema kwa ajili ya kupiga kambi.

Shuhuda mmoja amesema mamia ya waandamanaji walikuwa katika mahema wakati risasi za moto zilipoanza kumiminwa kutoka katika gari lililokuwa likipita. Kisha muda mchache baadae watu walio na silaha waliokuwa wamefunika nyuso zao waliwasili na kuanza kuwashambulia waandamanaji, kama anavyoongeza mwandamanaji huyu.

"Vikosi vya usalama vinarusha gesi ya kutoa machozi dhidi ya maandamano ya amani. Tunataka kubadili katiba na shughuli za serikali na hatutaki ushiriki wa vyama katika utawala mpya na serikali".

Karbala, Baghdad na miji mingine iliyoko kusini mwa Iraq imekumbwa na wimbi la maandamano ya umwagaji damu ambayo yamegeuka kuwa ghasia, huku maafisa wa usalama wakiwashambulia waandamanaji ambao nao wamekuwa wakiyachoma moto majengo ya serikali.

Maandamano ya mjini BaghdadPicha: Reuters/T. Al-Sudani

Maandamano hayo yamechochewa na hasira dhidi ya vitendo vya rushwa, kudorora kwa uchumi na huduma mbovu za serikali. Licha ya utajiri wake wa mafuta, Iraq inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na miundombinu mibovu, huku kukiwa na hali ya kukatika umeme mara kwa mara kunakowalazimisha watu kutumia majenereta.

Maandamano hayo yameshamiri na sasa waandamanaji wanataka mabadiliko ya haraka si tu serikali kujiuzulu. Waziri mkuu wa Iraq Adel Abdel-Mahdi ameahidi mabadiliko ya serikali sambamba na mpango wa mageuzi ambao umekataliwa tayari na waandamanaji.

Maelfu ya wanafunzi walijiunga na maandamano ya kupinga serikali siku ya Jumatatu baada ya kukwepa masomo katika vyuo vikuu na shule za sekondari.

Mamlaka zilitangaza marufuku ya kutotembea usiku katika mji mkuu wa Baghdad na katika majimbo mengine ili kukabiliana na maandamano yanayozidi kushika kasi. Kwa mujibu wa tume ya haki za binadamu ya Iraq, watu 80 wameuawa na maelfu kujeruhiwa kati ya Ijumaa na Jumatatu jioni. Ap/dpa

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW