1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 18 wauwawa katika shambulio Sahel

Hawa Bihoga
23 Februari 2022

Watu 18 wameuawa katika mashambulizi mawili katika makutano ya Niger, Burkina Faso na Mali. Waziri wa mambo ya ndani wa Niger amesema shambulio hilo limefanywa na watu wenye silaha ambao hadi sasa bado hawajatambuliwa.

Symbolbild Burkina Faso  Mehr als 138 Tote bei Anschlag
Picha: Michel Cattani/AFP

Shambulio hilo limetokea siku ya jumapili wakati watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha wakiwa katika pikipiki, walilishambulia lori lililokuwa likisafiri kati ya vijiji katika eneo la Tillaberi ambalo lipo katika makutano ya Niger,Burkina Faso na Mali.

Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani inasema kuwa, katika shambulio hilo jumla ya watu 18 waliuwawa, 4 walijeruhiwa huku 5 kati ya majeruhi 8, wamelazwa hopitalini wakiwa katika hali mbaya.

Soma zaidi:Senegal yaitaka Ujerumani kubakisha majeshi yake Mali

Taarifa imeongeza kuwa lori hilo lilichomwa moto na hadi sasa msako unaendelea ili kubaini washambuliaji.

Mbunge wa eneo hilo alisema kuwa,gari lililolengwa na washambuliaji lilikuwa likirejea kutoka mji mkuu wa Niger Niamey,likiwa na abiria kutoka vijiji vinne katika eneo hilo pamoja na mizigo yao.

Mashuhuda katika eneo hilo waliripoti kwamba washambuliaji waliwauwa karibu wanaume wote waliokuwa ndani ya gari hilo kabla ya kuchukua mizigo yao na kuchoma lori hilo moto.

Wakaazi mkoani Tallaberi katika mkutano wa pamojaPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Makundi yenye kujihami na silaha yalifanya mashambulizi mengi dhidi ya raia katika eneo hilo mwaka 2021,mwezi Oktoba mwaka uliopita washambuliaji waliokuwa katika pikipiki waliwauwa watu kumi katika msikiti  mmoja huko Tizigorou wakati wa sala ya jioni.

Soma zaidi:Machafuko Sahel yachangia njaa kwa mamilioni ya watu

Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi Jumatano iliyopita wanajeshi watano wa Niger waliuwawa katika mlipuko kusini magharibi mwa nchi ya Sahel. Mlipoko huo ulitokea katika wilaya ya Gotheye ya Tillaberi.

Kukithiri makundi ya wapiganaji.

Eneo la Magharibi mwa Niger kwa miaka mingi limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi, licha ya juhudi za vikosi vya kimataifa vilivyotumwa katika eneo la Sahel kupambana na waasi wenye itikadi kali.

Mwanajeshi akitazama jengo lililoharibiwa kwa shumbulio la Boko HaramPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Kulingana na ripoti ya maendeleo ya binadamu ya Umoja wa Mataifa Niger ni nchi masikini zaidi duniani na imekuwa ikikabiliana na makundi yenye itikadi kali kama vileBoko Haram na Dola la Kiislamu.

Mali taifa jirani na Niger, limekuwa likijitahidi kuzuia uasi wa kikatili wa wapiganai wa jihadi ambao uliibuka kwa mara ya kwanza mnamo 2012, kabla ya kuenea hadi Burkina Faso na Niger.

Maelfu ya wanajeshi na raia wameuawa na watu milioni mbili wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo wa Sahel kote, ambao Mali bado ndio kitovu chake.

Soma zaidi:Ufaransa na Washirika wake waamua kuondoka Mali

Wiki iliyopita Ufaransa ilitangaza kujiondoa kijeshi  kutokana na mzozo kati yake na utawala wa kijeshi wa Mali, ambao ulichukua mamlaka mwaka tangu 2020 na kukaidi wito wa kimataifa wa kurejesha utawala wa kiraia haraka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW