Watu 1,800 wafa kwa malaria Burundi
6 Agosti 2019Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema visa milioni 5.7 vya ugonjwa wa malaria vilirikodiwa nchini Burundi mnamo 2019, idadi hiyo ni sawa na nusu ya watu wote wanaoishi nchini Burundi.
Nchi hiyo ndogo katika ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika ina jumla ya watu milioni 11 na bado mpaka sasa haijatangaza dharura ya kitaifa, licha ya shirika la OCHA mnamo mwezi Mei kusema kwamba kuzuka kwa mripuko wa ugonjwa wa malaria ni janga.
Mpango wa kitaifa wa kuudhibiti ugonjwa wa malaria ambao kwa sasa umeanzishwa, umeonyesha kukosa rasilimali watu, vifaa na fedha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa OCHA katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu dharura ya kibinaadamu.
Shirika hilo limewataka wadau wote, pamoja na mamlaka ya kitaifa na washirika kuchangia rasilimali zinazohitajika kupambana na malaria kabla ya visa zaidi kuongezeka.