Watu 20 wauawa katika shambulizi la hoteli Mogadishu
22 Januari 2016Vikosi vya polisi vilifanikiwa kudhibiti mgahawa huwo kabla ya kuingia alfajiri, alisema Kapteni Mohamed Hussein, akiwa anazungumza katika eneo la mashambulizi, mjini Mogadishu, ingawa hakuweka wazi kama idadi hiyo ya watu 20 waliouawa inajumuisha pia washambuliaji.
Kupitia redio ya mtandaoni, Radio Andalus, wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamedai kuhusika na mashambulizi hayo.
“Nilikuwa na marafiki zangu watatu waliporipua kwa mara ya kwanza. Bahati nzuri nimesalimika lakini rafiki zangu wameuawa hapo hapo. Madirisha yalivunjwavunjwa na watu walikuwa wanakimbia huku na kule. Ilikuwa ni hali ya kusikitisha. Dunia gani hii tunayoishi sasa? Hakuna sehemu yoyote kulipo salama,” anasema Abdullahi Biid, kijana aliyeshuhudia tukio hilo.
Milio ya risasi ilihanikiza mjini humo wakati vikosi vya usalama vya Somalia vilipoingilia kati mashambulizi hayo na kukagua chumba hadi chumba cha mkahawa huo wakiwa wanawasaka wapiganaji wa al-Shabaab waliokuwa ndani.
Hussein amesema vikosi hivyo vimefanikiwa kuwaokoa watu kadhaa waliokuwa na sherehe ndani ya ukumbi wa mkahawa huwo wakati mashambulizi yalipoanza jana usiku.
Walioshuhudia tukio hilo wanasema, wanamgambo waliuvamia mgahawa wakitokea ufukweni, huku wakiwa wanapiga kelele "Allahu Akbar" neno la Kiarabu linalomaanisha Mungu Mkubwa.
Mashambulizi ya pili ndani ya wiki moja
Ahmed Nur, aliyeshuhudia tukio hilo wakati akiwa anatembea ufukweni, anaeleza kwamba washambuliaji hao walianza kurusha risasi wakiwa bado ufukweni kabla hawajaingia ndani ya mkahawa huo.
Haya ni mashambulizi ya pili makubwa ndani ya wiki moja kufanywa na kundi hilo ndani ya ardhi ya Somalia. Wiki iliyopita, wanamgambo hao waliivamia kambi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM) kusini mashariki mwa Somalia, ambapo walisema waliwauwa takribani wanajeshi 100 wa Kenya, kuwakamata wengine mateka na pia kuchukuwa silaha la magari yao ya kijeshi. Serikali ya Kenya bado haijatoa idadi rasmi ya waliouawa katika mashambulizi hayo.
Licha ya kuondoshwa katika miji na mitaa kadhaa nchini Somalia, bado al-Shabaab inaendelea kufanya mashambulizi kwenye maeneo tofauti katika Pembe ya Afrika, ikivilenga zaidi vikosi vya Umoja wa Afrika, maafisa wa serikali pamoja na wageni wa nchi tofauti.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape
Mhariri: Mohammed Khelef