Watu 200,000 huenda wakafa kwa corona, Marekani
30 Machi 2020Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza muda wa vizuizi vya dharura katika kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona nchini humo, ambako wanasayansi waandamizi wanaonya kwamba huenda hadi watu 200,000 wakafariki kutokana na maradhi yanayosababishwa na virusi hivyo vya mrdhi ya COVID-19.
Rais Trump aidha ameongeza muda wa watu kujitenga na mijumuiko hadi Aprili 30, akiachana na muda wa awali aliouweka wa zuio hilo ulioishia wakati wa sherehe za pasaka.
"Kwa hiyo kwa wiki mbili zijazo na katika kipindi hiki chote ni muhimu kwa kila mmoja kufuata kikamilifu miongozo, ambayo makamu wetu wa rais anaisisitizia sana. Anaiamini sana, kadiri tunavyofanya kwa haraka, ndivyo tutasaidia kulimaliza haraka jinamizi hili. Kwa hiyo, tutaongeza muda wa miongozo yetu hadi Aprili 30 ili kupunguza kasi ya maambukizi," alisema Trump.
Hatua hii ya Trump inakuja katika wakati ambapo Uingereza na Italia ambayo imeathiriwa pakubwa na virusi vya corona zikionya kwamba hatua za kupambana na kusambaa zaidi kwa virusi hivyo zitadumu kwa miezi kadhaa inayokuja, huku akionya kwamba mzozo huo utaendelea kuiathiri vibaya Marekani.
COVID-19 tayari imewaua watu zaidi ya 33,000 kote ulimwenguni, huku idadi ya visa vilivyothibitishwa ikikaribia 700,000.
Nchini Ujerumani, taasisi ya masuala ya afya ya umma na udhibiti wa magonjwa ya Robert-Koch imearifu mapema hii leo kwamba idadi ya walioambukuzwa imeongezeka hadi 57,298, baada ya kugunduliwa visa vipya 4,751. Vifo 66 vilivyoripotiwa vimefanya idadi ya waliokufa sasa kufikia 455.
Soma Zaidi: Imran Khan: Nchi maskini zitaathirika zaidi na Corona
Jiji la Moscow nchini Urusi limeanza utekelezaji wa amri ya kusimamisha shughuli kufuatia tangazo la ghafla la sheria mpya za meya wa jiji la hilo usiku wa jana. Meya Sergei Sobyan alitangaza sheria hizo baada ya wakaazi wa kupuuza ushauri rasmi wa kujitenga na mijumuiko katika siku za mwisho wa wiki.
Watakaoruhusiwa ni wafanyakazi wa shughuli zitakazotambuliwa kuwa muhimu, wanaotoka kununua vyakula na dawa na shughuli nyingine muhimu, lakini si umbali wa zaidi ya mita 100 kutoka kwenye makaazi yao.
India imesema haitaogeza muda wa kusimamisha kabisa shughuli nchini humo, hii ikiwa ni kulingana na serikali hii leo. Hatua yake hiyo iliyoshuhudia watu bilioni 1.3 wakishindwa kufanya shughuli za kila siku ili kujikimu inahitimishwa Aprili 15 wakati kukiwa na visa 1,071 na vifo 29.
Nchini Israel, msaidizi wa waziri mkuu, Benjamin Netanyahu amekutwa na maambukizi ya virusi hivyo, hatua inayoiweka mashakani afya ya waziri mkuu mwenye miaka 70. Hata hivyo vyombo vya habari vimesema msaidizi huyo anaendelea vizuri.
Huku hayo yakiendelea, huko Belarus rais Alexander Lukashenko amepuuzilia mbali janga la corona na hata kuwahimiza watu wake kuendelea na biashara kama kawaida, akidai kwamba shughuli zinazofanywa kwa kutumia matrekta na mashambani zina uwezo wa kuwasaidia wakulima kupona na janga hilo.
Mashirika: DW