Watu 21 wahukumiwa kifo Misri
26 Januari 2013Watu sabini na tatu wakiwemo maafisa wa michezo na polisi wanashtakiwa kwa madai ya mauaji ya kudhamiria au uzembe kuhusiana na ghasia hizo zilizotokea kwenye uwanja wa Port Said hapo mwezi wa Februari.
Ghasia hizo zilizuka kati ya mashabiki hasimu wa timu wenyeji wa pambano hilo Al Masry na Al-Ahly wakati wa michuano ya ligi kuu na kusababisha watu 74 kupoteza maisha yao.Hayo yalikuwa ni maafa makubwa kuhusiana na mchezo wa mpira wa miguu kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Polisi wawili ni miongoni mwa watu waliouwawa katika ghasia za Jumamosi na kwa mujibu wa mkurugenzi wa afya katika mji wa Port Said watu zaidi ya 200 wamejeruhiwa.
Washitakiwa wengine kuhukumiwa Machi
Hakimu wa mahakama amesema hukumu kwa washtakiwa wengine 52 waliobakia itatolewa tarehe tisa mwezi wa Machi. Kutokana na sababu za usalama takriban washtakiwa wote hawakuwako mahakamani mjini Cairo wakati hukumu hiyo ilipotolewa.
Washtakiwa wote wana haki ya kukata rufaa na kati ya wale waliohukumiwa Jumamosi hakuna askari yoyote.
Mahakama ya Cairo iliotowa hukumu hiyo sasa imeikabishi kwa kiongozi wa juu wa dini nchini humo kwa maoni ya mwisho.Utekelezaji wa hukumu za adhabu za kifo nchini Misri lazima uidinishwe na Mufti Mkuu.
Katika mji wa Port Said kumezuka mapambano kati ya waandamanaji na polisi. Mashabiki wa timu ya Al-Masry na familia za washtakiwa wanasema kulikuwa na mkono wa kisiasa katika kesi hiyo.
Polisi ilitumia gesi ya kutowa machozi kutawanya waandamanaji ambao walijaribu kulivamia gereza wanakoshikiliwa washtakiwa.
Timu ya Al-Ahly yasherehekea hukumu
Hata hivyo mamia ya mashabiki wa timu ya Al-Ahly walisherehekea hukumu hiyo kwa kuwasha fataki na kuimba nyimbo katika mitaa ya Cairo. Kulikuweko na nderemo ndani na nje ya mahakama katika mji mkuu huo wakati hukumu hiyo ikisomwa mahakamani.Wanawake walipiga vigeregere,familia na jamaa za wahanga walikumbatina na kupiga mayowe ya "Allahu Akbar".
Mapambano ya Port Said yamepelekea kuwekwa kwa wanajeshi katika mji huo kulinda taasisi muhimu za serikali na kurudisha usalama.
Vituo viwili vya polisi vilivamiwa na milio mizito ya risasi ilikuwa inasikikika kutoka kitongoji cha Al Manakh.Magari ya kubebea wagonjwa yamekuwa yakipeleka majeruhi hospitali na maduka na shughuli zote za biashara zilifungwa wakati waandamanaji wakiunguza mipira barabarani.Misikiti katika mji huo imekuwa ikitowa wito kwa watu kujitolea damu.
Uamuzi huo umekuja masaa machache baada ya vikosi kuwekwa katika mji wa karibu wa mwambao wa Suez kufuatia mapambano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga serikali kusababisha vifo vya watu tisa.
Mapambano ya Suez ni mabaya kabisa katika wimbi la ghasia lililozuka nchini kote Misri hapo Ijumaa wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya vuguvgu lilimn'gowa madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.
Muungano wa Ukombozi wa Taifa ambao ni muungano mkuu wa upinzani wa vyama na makundi ya vuguvugu wenye kupinga utawala wa Waislamu wa itikadi kali nchini humo umetowa wito miongoni mwa mambo mengine kuundwa kwa serikali ya ukombozi wa taifa venginevyo hautoshiriki katika uchaguzi ujao wa bunge.
Rais Mohamed Mursi ametowa wito wa kuwepo kwa utulivu na kuahidi kwamba serikali itawafikisha mbele ya sheria wale wenye kuvunja sheria za nchi hiyo. Ametaka watu waheshimu misingi ya mapinduzi ya Misri na kutowa maoni yao kwa uhuru na kwa amani.
Mwandishi : Mohamed Dahman/afp/dpa
Mhariri: Sudi Mnette