Watu 24 wapoteza maisha baada ya bwawa kupasuka Kenya
29 Aprili 2024Kulingana na gavana wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika, idadi hiyo ni makadirio. Miili zaidi inahofiwa kukwama kwenye tope wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.
Bwawa hilo linakiswa kuvunja kingo zake mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia leo baada ya kujaa maji ya mvua kubwa inayozidi kunyesha.
Maji hayo yalisambaa kwenye mitaa iliyo karibu na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa. Aidha maji hayo yameharibu barabara kuu ya Nairobi- Nakuru na kuyasomba magari ya uchukuzi.
Magari matano ya uchukuzi yalisombwa na maji likiwemo basi lililokuwa na watu 60, hata hivyo hatma ya abiria hao haijulikani.
Kufuatia hali hiyo serikali ya Kenya imeahirisha ratiba ya kufungua shule baada ya likizo kote nchini hadi tarehe sita mwezi ujao. Shule zilitarajiwa kufunguliwa leo.