1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Watu 25 wauawa katika mashambulizi ya Gaza

11 Mei 2023

Mashambulizi ya anga na makombora yaliyorushwa kutoka Israel yamewaua Wapalestina 25 tangu siku ya Jumanne, wakiwemo wapiganaji na raia, wakati ambapo jeshi la Israel na wanamgambo wa Gaza wakiendeleza mapambano makali.

Palästina Israel | Konflikt | Nach Angriffen auf Gaza
Picha: JINI/Xinhua/IMAGO

Jeshi la Israel limesema kuwa zaidi ya roketi 500 zimerushwa kutoka Gaza kuelekea Israel tangu siku ya Jumanne, ingawa hakuna vifo wala majeruhiwa walioripotiwa kwa upande wa Israel hadi sasa.

Miongoni mwa roketi hizo, 368 zilivuka mpaka na 154 ziliharibiwa kwa mfumo wa kujilinda na makombora wa Israel wa Iron Dome, huku roketi 110 zikiangukia ndani ya Gaza.

Israel yalilishambulia kundi la Islamic Jihad

Mapema Alhamisi jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la wanamgambo wa Islamic Jihad katika eneo la pwani ya Palestina na limesema kwamba kamanda wa ngazi ya juu wa kundi hilo anayehusika na kikosi cha kufyatua makombora, Ali Ghali ameuawa baada ya makaazi yake kushambuliwa.

Kundi jingine la wanamgambo la Popular Front for the Liberation of Palestine, limesema kuwa wapiganaji wake wanne wameuawa.

Wanawake wa Kipalestina wakiwa nje ya nyumba iliyoharibiwa baada ya mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Akilihutubia taifa Jumatano usiku kwa njia ya televisheni, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema kuwa bado wako katikati ya kampeni na wanaushambulia vikali Ukanda wa Gaza. ''Kampeni bado haijamalizika, tutaendelea kuwapa taarifa. Tumeingia kwenye hili pamoja, tutavuka pamoja na tutashinda pamoja,'' alisisitiza Netanyahu.

Netanyahu amerudia kusema kuwa yeyote yule anayewadhuru na anayewatuma magaidi dhidi yao, atalipia hayo yanayoendelea. Amesema anawaona magaidi wote na hawawezi kujificha.

Guterres alaani mauaji ya raia Gaza

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali mauaji ya raia huko Gaza, wakiwemo wanawake watano na watoto watano, akisema kuwa hayakubaliki na amezitaka pande zote kujizuia.

Kwa mujibu wa naibu msemaji wa umoja huo, Farhan Haq, Guterres amesema Israel inapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu kwa kuchukua tahadhari zote zinazowezekana kuwalinda na kuwaokoa raia pamoja na miundombinu ya kiraia wakati wanapoendelea na operesheni za kijeshi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: FEISAL OMAR/REUTERS

Guterres pia amelaani kurushwa kiholela kwa makombora kutoka Gaza kwenda Israel, hatua ambayo inakiuka sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kuwaweka hatarini raia wa Palestina na Israel.

Mashambulizi ya anga ya Israel yamekosolewa na Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammed Shtayyeh, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan na serikali ya Misri, ambao mara nyingi wamekuwa wapatanishi kati ya Israel na makundi ya wanamgambo ya Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.

Jumuia ya Nchi za Kiarabu, Arab League, imelaani vikali mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, ikisema kuwa ni ya kinyama na ambayo yamewalenga raia, wanawake na watoto katika maeneo ya makaazi. Nao Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi mkubwa kutokana na hali inayoendelea Gaza na unasikitishwa na mauaji ya raia.

(AP, DPA, AFP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW