Watu 26 wauwawa Pakistan siku moja kabla ya uchaguzi
7 Februari 2024Shambulizi la kwanza lililowaua watu 14 lilitokea katika ofisi ya mgombea binafsi katika mji wa Pishin, huku shambulio la pili katika eneo la Qilla Saifullah, karibu na mpaka wa Afghanistan, ilitokea karibu na ofisi ya Jamiat Ulema Islam JUI, chama cha kidini ambacho awali kililengwa katika mashambulizi ya wanamgambo ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wa habari wa eneo hilo.
Naibu kamishna wa mji wa Qilla Saifullah, Yasir Bazai, amesema watu 12 waliuwawa na wengine 25 kujeruhiwa baada ya vilipuzi vilivyowekwa katika pikipiki iliyokuwa imeegeshwa karibu na ofisi hiyo, kuripuka.
Hata hivyo mpaka sasa haijawa wazi ni kina nani hasa waliohusika na shambulizi hilo. Lakini makundi kadhaa likiwemo kundi la wanamgambo wa Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) na kundi la watu wanaotaka kujitenga la Balochistan wanapinga dola la pakistan, wamekuwa wakifanya mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni.
Serikali yasema inaimarisha usalama katika vituo vyote vya kupigia kura
Haya yote yanafanyika wakati Pakistan, ikishiriki uchaguzi hapo kesho Alhamisi (08.02.2024) licha ya mashambulizi hayo ya wanamgambo na pia kufungwa jela kwa Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan, aliyekuwa mshindi wa uchaguzi uliomalizika Pakistan, ambaye amekuwa akivuma katika vichwa vya habari licha ya mgogoro wa kiuchumi na masuala mengine yanayoitishia nchi hiyo iliyo na silaha za nyuklia. Serikali imeahidi kuimarisha usalama katika vituo vya kupigia kura.
Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Pakistan, mpaka wake wa upande wa Magharibi unaopakana na Iran na Aghanistan utafungwa na kufunguliwa siku ya Ijumaa ili kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wa uchaguzi.
Balozi wa Pakistan nchini Uingereza Jane Marriott, amesema ameshitushwa na shambulio aliloliita la kigaidi na kuwakosoa wale aliyosema wana nia ya kuwazuwia watu kujitokeza kupiga kura.
Kaimu Waziri Mkuu Anwaarul-Haq-Kakar amekosoa mashambulizi hayo pia na kutoa salamu za rambirambi kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao. Amesema kila jaribio la kukwamisha utawala wa kisheria litashindwa na kwamba serikali ina nia ya kuandaa uchaguzi wa amani. Msemaji wa serikali Achakzai ametangaza siku tatu za maombolezo lakini akasisitiza kwamba uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa na kutoa wito kwa watu wa Pakistan kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura na kuwashinda wale waliotaka kuchelewesha mchakato mzima wa uchaguzi.
Chanzo: afp/ap/reutes