Watu 29 wauwawa Istanbul
11 Desemba 2016Mabomu hayo yalilenga maafisa wa polisi , na kuwauwa 27 kati yao pamoja na raia wawili, waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki, Suleyman Soylu aliwaambia waandishi habari mapema leo Jumapili. Ameongeza kuwa watu 10 wamekamatwa kwa kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.
Vifo vya raia vilikuwa chini kwasababu mashabiki walikuwa wamekwisha ondoka katika uwanja huo mpya wa Vodafone Arena baada ya mchezo wa mpira wakati mripuko huo wa bomu ulipotokea. Watu walioshuhudia pia walisikia milio ya bunduki baada ya mripuko.
"Kwa mara nyingine tumeshuhudia usiku wa leo upande mwingine wa taswira mbaya ya ugaidi ambayo inakanyaga kila maadili na utu," rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema katika taarifa.
Bomu la kwanza liliripuka nje ya uwanja maarufu unaofahamika kama Besiktas baada ya timu ya eneo hilo kucheza na timu ya jirani. Mripuko wa pili ilikuwa muda mfupi baadaye na ulielezwa na maafisa kuwa ni shambulizi la kujitoa muhanga.
Shambulio la kigaidi
Polisi walilifunga eneo hilo huku moshi ukifuka kutoka nyuma ya uwanja huo na magari ya kubebea wagonjwa yalianza kuwapeleka watu waliojeruhiwa hospitali. Vioo kutoka katika madirisha yaliyovunjika vya majengo ya karibu vilitapakaa katika sehemu ya wapita kwa miguu.
Hakuna kundi ambalo lilitangaza kuhusika na shambulio hilo mara moja. Mwaka huu, mji wa Istanbul umeshuhudia ongezeko la mashambulio ambayo maafisa wanasema yanafanywa na kundi la Dola la Kiislamu ama kudaiwa kufanywa na wanamgambo wa Kikurdi.
Hali ya hatari imewekwa kufuatia jaribio lililoshindwa la mapinduzi Julai 15.
Soylu alikiri kwamba nchi hiyo inasumbuka kuweza kupambana na makundi kadhaa, yanayojaribu kukandamiza mapambano yake dhidi ya ugaidi.
Uturuki ni mshirika katika muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu na majeshi yake yako katika nchi jirani za Syria na Iraq yakipambana na makundi kadhaa ya waasi na Dola la Kiislamu.
Pia nchi hiyo inakabiliana na mzozo mpya na kundi lililopigwa marufuku la Wakurdi upande wa kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Ned Price , msemaji wa baraza la usalama wa taifa nchini Marekani , amesema Marekani inalaani shambulio hilo , kwa kiwango cha juu kabisa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Yusra Buwayhid