Idadi ya vifo Uturuki na Syria yapindukia 33,000
13 Februari 2023Huku Umoja wa Mataifa ukikaridia kuwa zaidi ya watu 33,000 wamekufa hadi sasa, mvulana mwenye umri wa miaka saba na mwanamke mwenye umri wa miaka 62 wameokolewa mapema Jumatatu asubuhi baada ya kukwama kwenye kifusi kwa takribani siku saba.
Mvulana huyo anayeitwa Mustafa ameokolewa katika jimbo la Hatay kusini mashariki mwa Uturuki, huku Nagize Yilmaz akiokolewa katika mji wa Nurdagi kwenye jimbo hilo hilo pia ikiwa ni wiki moja imepita tangu yalipotokea matetemeko hayo.
Matumaini ya kuwapata watu zaidi wakiwa hai yanafifia
Shirika la majanga la Uturuki, AFAD limesema zaidi ya watu 32,000 kutoka mashirika ya Kituruki yanaendelea na juhudi za kuwatafuta na kuwaokoa watu wakishirikiana na timu ya maafisa wa uokozi 8,294 wa kimataifa.
Jana, timu za uokozi kutoka Urusi, Kyrgyzstan na Belarus zilifanikiwa kumtoa mwanaume mmoja akiwa hai kutoka kwenye jengo lililoanguka nchini Uturuki, baada ya kukwama kwenye kifusi kwa muda wa saa 160. Hata hivyo, waokozi wanasema kuwa matumaini ya kuwapata watu wengine zaidi wakiwa hai yanafifia.
Huku idadi ya watu waliokufa nchini Uturuki ikifikia 29,605, zaidi ya watu 4,300 wamekufa nchini Syria, na wengine zaidi ya 7,600 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa AFAD, kati ya Jumatatu na Jumamosi, matetemeko mengine madogo zaidi ya 2,000 yametokea.
Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo la mpaka wa Uturuki na Syria wa Bab al-Hawa, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu na masuala ya dharura, Martin Griffiths amesema anatarajia idadi ya vifo itaongezeka na kuzidi 50,000.
Misaada yanza kuingia Syria
Griffiths ambaye siku ya Jumamosi aliwasili kusini mwa Uturuki kutathmini uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo, amesema misaada ya kiutu inaendelea kutolewa na mingine imeanza kupelekwa kaskazini magharibi mwa Syria.
''Tunachokiona hapa ni msafara wa misaada ya kiutu. Kila siku kuna msafara unaenda, kuna takribani malori 10 yanayopeleka mahitaji ya dharura ya kiutu kwa watu wa kaskazini mashariki mwa Syria. Zaidi ya watu milioni nne wanahitaji msaada wetu,'' alifafanua Griffiths.
Griffiths ambaye Jumatatu amelizuru eneo la Aleppo nchini Syria, amesema dharura sasa imeelekezwa kwenye kutoa makaazi, chakula, shule na huduma ya kisaikolojia kwa watu walioathiriwa na matetemeko hayo ya ardhi. Amesema Umoja wa Mataifa utapeleka misaada kwenye maeneo ya kaskazini magharibi mwa Syria yanayodhibitiwa na waasi, ambayo pia yameathirika vibaya na matetemeko hayo.
Erdogan awaonya waporaji
Wakaazi na wafanyakazi wa mashiriki ya kutoa misaada kutoka kwenye miji mingine ambao walikwenda kwenye mji wa Antakya ulioathirika zaidi wameshuhudia kuzorota kwa hali ya usalama, huku matukio ya wizi na uporaji yakiendelea kwenye maduka na nyumba zilizobomolewa kwa matetemeko ya ardhi. Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema serikali yake itawachukulia hatua kali watu watakaobainika kuhusika na uhalifu huo.
Wakati huo huo, maafisa wa Uturuki wameamuru kukamatwa kwa wakandarasi 113, wanaotuhumiwa kuhusika katika ujenzi wa baadhi ya majengo ambayo yameporomoka wakati wa matetemeko hayo. Makamu wa Rais, Fuat Oktay amesema watuhumiwa 131 wametambuliwa na 113 kati yao wamekamatwa.
(AFP, DPA, AP, Reuters)