27 Desemba 2016
Mauaji ya watu yalifanyika katika mji wa Eringeti, ulioko kilomita 55 kaskazini mwa mkoa wa Beni ambao kwa kipindi cha miaka miwili umekuwa katika machafuko yaliyowaua mamia ya watu. Waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), waliwaua watu 22 baada ya kuvamia mji wa Eringeti Jumamosi iliyopita. Afisa mmoja wa eneo hilo, Amisi Kalonda, alilieleza shirika la habari la AFP. Idadi ya vifo iliongezeka na kufikia 35 hapo jana baada ya kupatikana taarifa kuwa kiasi ya watu 13 wa kabila la Hutu wengi wao wakiwa ni wanawake na mtoto wa kike wa umri wa miaka minane waliuawa hapo Jumapili na wapiganaji wa kabila la Nande. Watu wa kabila la Nande na makabila mengine nchini humo, wanawachukulia Wahutu kama wageni kwa sababu ya kujiambatanisha kwao na kabila lenye watu wengi katika nchi ya jirani ya Rwanda.