1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 37 wahukumiwa kifo kwa jaribio la mapinduzi DRC

14 Septemba 2024

Mahakama ya Kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwahukumu kifo watu 37, wakiwemo raia watatu wa Marekani, baada ya kuwatia hatiani kwenye mashitaka ya kushiriki katika jaribio la mapinduzi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Mapinduzi ya Kijeshi | Kinshasa
Waasi waliojaribu kufanya mapinduzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo tarehe 19 Mei 2024.Picha: Christian Malanga/Handout/REUTERS

Akisoma hukumu hiyo siku ya Ijumaa (Septemba 13) mjini Kinshasa, Jaji Meja Freddy Ehuma alisema watuhumiwa hao wanapewa "adhabu kali kabisa, adhabu ya kifo".

Raia hao watatu wa Wamarekani, wakiwa wamevalia sare za buluu kwa manjano za jela na wakiwa wamekaa kwenye viti vya plastiki, walionekana wakiwa wameduwaa wakati mkalimani akiwaelezea hukumu yao iliyosomwa kwa lugha ya Kifaransa na Jaji Ehuma.

Mbali na raia hao wa Marekani, kulikuwapo pia raia mmoja wa Uingereza, mmoja wa Ubelgiji na mmoja wa Kanada. 

Wote kwa pamoja wana siku tano za kukata rufaa kwa hukumu hiyo ambayo ilijumuisha mashitaka ya jaribio la mapinduzi, ugaidi na kujihusisha na uhalifu. Watuhumiwa 14 waliachiliwa huru kwenye kesi hiyo iliyoanza mwezi Juni.

Soma zaidi: Mahakama Kongo yawahukumu kifo watu 37 waliojaribu mapinduzi

Wakili wa raia hao sita wa kigeni, Richard Bondo, alipinga uwezekano wa hukumu ya kifo kuweza kutekelezwa kwa sasa nchini Kongo, licha ya kurejeshwa tena mapema mwaka huu na alisema wateja wake walikuwa na wakalimani wasiokuwa na uwezo wakati kesi hiyo ilipokuwa ikichunguzwa.

"Tutapinga uamuzi huu kwa kukata rufaa," alisema Bondo.

Watu sita waliuawa wakati wa jaribio hilo la mapinduzi lililoongozwa na kiongozi wa upinzani asiyefahamika sana, Christian Malanga, mnamo mwezi Mei, ambaye aliyalenga makaazi ya Rais Felix Tshisekedi na mshirika wake wa karibu, Vital Kamerhe, ambaye kwa sasa ndiye spika wa bunge.

Jeshi la Kongo lilisema Malanga mwenyewe aliuawa kwenye makabiliano muda mfupi baada ya kutangaza mashambulizi yake moja kwa moja kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

Mtoto wa kiongozi wa jaribio 

Mtoto wake wa kiume, Marcel Malanga mwenye umri wa miaka 21 na ambaye ni raia wa Marekani, ni miongoni mwa Wamarekani watatu waliotiwa hatiani na mahakama ya kijeshi. Aliiambia mahakama kuwa baba yake alikuwa amemlazimisha yeye na rafiki yake waliyekuwa pamoja skuli ya sekondari ya juu kushiriki kwenye mashambulizi hayo.

Vital Kamerhe, mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi.Picha: Arsene Mpiana/AFP

"Baba alitutishia kutuua kama hakutufuata amri zake," alisema Marcel mahakamani hapo.

Soma zaidi: Kongo kuendelea na kesi dhidi ya jaribio la mapinduzi

Watuhumiwa wengine kwenye kundi hilo la wanamgambo walizungumzia vitisho kama hivyo kutoka kwa Malanga, na wengine walielezea kughilibiwa wakiamini kwamba walikwua wanafanyia kazi shirika la kujitolea.

Mama yake Marcel, Brittney Sawyer, anashikilia kuwa mwanawe hana hatia na kwamba alikuwa akimfuata tu baba yake, ambaye alikuwa akijichukulia mwenyewe kuwa rais wa serikali kivuli iliyo uhamishoni.

Kwa kipindi chote tangu mwanawe akamatwe, alikuwa akitumia muda wake mwingi kukusanya fedha za kumtumia ili apate chakula, vifaa vya usafi na kitanda. Marcel alikuwa akilala sakafuni katika jela ya kijeshi ya Ndolo na amepata maradhi ya ini, kwa mujibu wa mama huyo.

Wamarekani wengine ni Tyler Thompson Jr. mwenye umri wa miaka 21, ambaye alisafiri kwenda Afrika akitokea Utah pamoja na Marcel kwa kile ambacho familia yake iliamini kuwa mapumziko ya bure, na Benjamin Reuben Zalman-Poulon mwenye umri wa miaka 36, ambaye anaripotiwa kufahamiana na Christian Malanga kupitia kampuni ya uchimbaji dhahabu.

Kampuni hiyo ilianzishwa nchini Msumbiji mwaka 2022 kwa mujibu wa jarida linalochapishwa na serikali ya Msumbiji na ripoti ya jarida la Africa Intelligence.

Serikali ya Marekani kutoingilia kati

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Matthew Miller, aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington siku ya Ijumaa kwamba serikali ya nchi yake ilikuwa inajuwa kuhusu hukumu hiyo- Wizara hiyo haikusema ikiwa Wamarekani hao watatu wamekamatwa kinyume na sheria, jambo ambalo linaonesha huenda maafisa wa Marekani hawatapigania kurejeshwa kwao nyumbani.

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: DW

"Tunafahamu kuwa mchakato wa kisheria nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaruhusu watuhumiwa kuukatia rufaa uamuzi wa mahakama," alisema Miller. "Wafanyakazi wa ubalozi wamekuwa wakihudhuria kwenye kesi muda wote. Tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu."

Soma zaidi: Kesi ya jaribio la 'mapinduzi' yaanza kusilikzwa Kongo

Thompson alikuwa amealikwa kwenye safari hiyo ya Afrika na Marcel, ambaye walikuwa pamoja kwenye timu ya mpira ya skuli yake katika kiunga cha Salt Lake City, lakini ratiba ilisema wangefanya zaidi ya matembezi.

Wachezaji wengine wa timu hiyo wanadai kuwa Marcel alimpa Thomson hadi dola za Kimarekani 100,000 ili kujiunga na kazi ya ulinzi nchini Kongo, na kwamba alikuwa anataka sana kumchukuwa rafiki wa Kimarekani kwenye safari hiyo.

Familia ya Thomson inashikilia kwamba mtoto wao hakuwa akijuwa chochote kuhusu nia ya Marcel, hakuwa na mipango yoyote ya mambo ya kisiasa na hata hakupanga kuingia nchini Kongo. Yeye na Marcel walikuwa waende Afrika Kusini na Eswatini, kwa mujibu wa mama yake wa kambu, Miranda Thompson.

AP/dpa