Watu 37 wauawa Gaza katika shambulizi la Israel
6 Juni 2024Shambulizi baya lililowauwa watu 37 limetokea wakati wapatanishi wa vita vya Gaza, ambao ni Marekani, Qatar na Misri, wameanza tena mazungumzo yenye lengo la kupata makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka katika vita hivyo ambavyo vimedumu kwa takribani miezi minane.
Soma pia:Israel yaendelea kuishambulia eneo la Bureij Gaza
Jeshi la Israel limesema limewaangamiza wanamgambo kadhaa katika shambulizi hilo waliokuwa ndani ya shule hiyo inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina,UNRWA,katika eneo la Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Israel yalishtumu kundi la Hamas kwa kutumia vibaya miundombinu ya kiraia
Israel inalishtumu kundi la Hamas na washirika wake huko Gaza kwa kutumia shule, hospitali na miundombinu mingine ya kiraia ikiwa ni pamoja na vituo vinavyoendeshwa na UNRWA, kama vituo vya operesheni zake, madai ambayo yamekanushwa na kundi hilo.
Uhispania yajiunga na kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya ICC
Uhispania hivi leo limekuwa taifa la pili la Umoja wa Ulaya baada ya Ireland kujiunga na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika mahakama ya ICC. Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Jose Manuel Albares.
Wakati wa mkutano na waandishi habari, Albares amesema lengo lao kuu ni kumaliza vita na kufungua njia ya kupatikana kwa suluhisho la mataifa mawili.
Matamshi yake yanakuja wiki moja baada ya nchi hiyo, Ireland na Norway kulitambua taifa la Palestina na kuzua ghadhabu kutoka Israel.
Chile na Mexico pia zilikwishajiunga na kesi hiyo ya Afrika Kusini.
Mwanajeshi wa Israel auawa katika shambulizi la Hezbollah
Jeshi la Israel limesema leo kuwa afisa wake mmoja ameuawa katika eneo la kaskazini ambapo vikosi vyake vinahusika katika mapigano ya mpakani ya karibu kila siku na kundi la wanamgambo la Hezbollah nchini Lebanon.
Soma piaShambulizi la Israel nchini Lebanon lawaua watu watatu
Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema kuwa mwanajeshi huyo aliyetambulishwa Sajenti Refael Kauders mwenye umri wa miaka 39 aliuawa baada ya droni mbili kurushwa kutoka Lebanon kuelekea katika mji wa Hurfeish nchini Israel.
Kulingana na jeshi la Israel, tangu mapigano kuzuka kati yake na kundi la Hezbollah baada ya kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, idadi ya wanajeshi wake waliouawa imefikia 15 pamoja na raia 11.