Watu 5 wajeruhiwa Afghanistan
22 Februari 2012Waandamanaji mjini Kabul wamechoma moto ua la nyumba moja inayokaliwa na wageni, hii ikiwa ni siku ya pili ya maandamano baada ya nakala za kitabu kitakatifu cha Koran, kuchomwa moto katika kituo cha jumuiya ya Nato.
Kulingana na walioshuhudia, moto huo ulisambaa na kuteketeza eneo dogo la nyumba hiyo panapokaliwa wageni zaidi ya1500. Zaidi ya waandamanaji 26 walijeruhiwa katika kisa hicho.
Katika mji wa Jalalabad mashariki mwa Afghanistan, mtu mmoja ameuwawa na wengine kumi kujeruhiwa baada ya polisi kuwafyetulia risasi waandamanaji wanaopinga kuchomwa kwa nakala hizo za Qoran. Ahmad Ali said daktari katika hospitali ya eneo hilo amesema aliyeuwawa ni kijana mdogo huku akisema watu hao 10 waliopata majeraha ya risasi wanapata matibabu katika hospitali ya Jalalabad.
Kwa sasa polisi nchini humo wanajaribu kuwatawanya waandamanaji hao waliojawa na hamaki huku wakisema kwa sauti kuwa "kifo kwa Marekani".
Marekani yaomba msamaha.
Awali Marekani iliomba radhi kwa tukio hilo ikisema kwamba nakala hizo zilichomwa kwa bahati mbaya. Kamanda wa kikosi cha Kimataifa cha kulinda amani Afghanistan, ISAF, John Allen, amesema kamwe hawakukusudia kuchoma nakala hizo na si nia yao kuwaudhi waislamu kwa njia yoyote.
Leo mkuu wa polisi wa mjini Kabul, Mohammad Ayub Salangi, alifika katika eneo la maandamano na vikosi vyengine kadhaa ili kujaribu kuwatuliza waandamanaji. Daktari aliyezungumza na wanahabari lakini kwa njia ya siri amesema mtu mmoja aliyepigwa risasi yuko katika hali mbaya.
Kilometa kadhaa kutoka eneo la maandamano watu wengine walikusanyika karibu na kituo cha jeshi la Marekani na walikuwa wakirusha mawe. Baada ya tukio hilo la kuchomwa kwa Qoran kuwekwa wazi hapo jana zaidi ya waandamanaji 2,000 walimiminika barabarani wakipinga tukio hilo.
Mwandishi Amina Abubakar/AFPE/APE
Mhariri Josephat Charo