1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 50 wauawa, zaidi ya 200 wajeruhiwa kwenye mkanyagano

Sylvia Mwehozi
7 Januari 2020

Idadi ya watu waliofariki katika mkanyagano wakati wa mazishi ya kamanda wa kijeshi wa Iran Qassem Soleimani imefikia watu 50 huku wale waliojeruhiwa wakipindukia 200 na kulazimika kuahirisha mazishi ya kamanda huyo.

Iran Begräbnis von General Soleimani in Kerman
Picha: Reuters/Fars News Agency/M. Bolourian

Mashirika mawili ya habari ya nchini humo yamemnukuu mkuu wa huduma za dharura wa Iran Pirhossein Koulivand aliyesema waliouawa wamefikia 50 huku wengine 213 wakijeruhiwa. Mkanyaganohuo ulitokea muda mchache kabla ya kuzikwa kwa kamanda Soleimani, ambaye kifo chake kimeongeza vikali mvutano baina ya Tehran na Washington. Majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali kwa matibabu zaidi, lakini chanzo cha mkasa huo ni umati mkubwa uliojitokeza mtaani.

Vidio zilizosambaa awali mitandaoni zilionyesha miili ya watu ikiwa imezagaa barabarani huku watu wengine wakipaza sauti za kuomba msaada. Kutokana na mkasa huo mamlaka zililazimika kuahirisha shughuli ya mazishi ingawa hapakutolewa muda wa hadi saa ngapi kamanda huyo angezikwa.

Ripoti za awali zilisema kwamba makumi kwa maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika katika mji wa Kerman kutoa heshima zao za mwisho kwa Soleimani. Soleimani alikuwa kamanda wa kikosi cha Quds ambacho ni sehemu ya kikosi cha walinzi wa mapinduzi.

Umati mkubwa wa waombolezaji mjini KermanPicha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Kiongozi mkuu wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei ameamuru bajeti ya kikosi hicho kuongezwa kwa wastani wa Dola milioni 225 hadi kufikia mwezi Machi, kwa mujibu wa spika wa bunge.

Ongezeko hilo la bajeti linahusishwa na utekelezaji wa mipango ya ulipaji "kisasi kikubwa" dhidi ya Marekani iliyomuua Soleimani. Pia bunge la Iran limewaorodhesha makamanda wote wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon waliohusika kwenye mauaji hayo kuwa "magaidi". Mkuu wa kamati ya bunge ya usalama wa kitaifa Mojtaba Zonnour amethibitisha taarifa hizo.

"Kulingana na tathmini, waziri wa ulinzi na Trump mwenyewe wote ni magaidi na wataadhibiwa. Na kipengele cha tatu cha muswada wa dharura wa leo kilihusu uidhinishwaji wa euro milioni 200 wa kikosi cha al-quds na kitaidhinishwa", alisema mkuu huyo. 

Mwili wa Soleimani anayechukuliwa kama shujaa kwa Wairan walio wengi, ulipelekwa nchini Iraq na miji mingine ya Iran kabla ya kufikishwa mjini Kerman ambako ndiko alikozaliwa. Huko kote ulikopitishwa, idadi kubwa ya watu walimiminika mitaani na kupaza sauti za kuilaani Marekani.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW