1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 503 wauwawa Kharkiv, Ukraine

15 Aprili 2022

Mamlaka ya jimbo la Kharkiv imesema takribani watu 503 wameuwawa katika jimbo hilo tangu Urusi ianze uvamizi wake. Kupitia ukurasa wake wa telegram, Gavana Oleg Synegubov amesema idadi hiyo inahusisha watoto 24.

Ukraine | Zerstörung nach Angriffen in Charkiw
Picha: Privat

Gavana huyo amesema katika kipindi kifupi kilichopita majeshi ya Urusi yamefanya mashambulizi ya roketi 24 na vifaru karibu katika maeneo yote ya Kharkiv na kusababisha raia mmoja kuuwawa na wengine wanane kujeruhiwa.

Kharkiv ni mji wa pili kwa ukubwa kwa Ukraine, ambao kabla ya vita ulikuwa na jumla ya watu milioni 1.5. Mji huo ambao upo umbali wa kilometa 40 kutoka katika mpaka wa Urusi, umekuwa ukikabiliwa na mashambulizi ya majeshi ya Urusi ingawa wameshindwa kuudhibiti.

Katika hatua nyingine Rais wa Ukraine leo hii amewashukuru raia wa Ukraine kwa ustahimilivu wakati taifa hilo likitimiza siku 50 katika makabilioano makali na taifa jirani la Urusi. Rais huyo kadhalika ameyashukuru mataifa rafiki katika kipindi hiki cha vita.

Meli ya Urusi iliyodaiwa kushambuliwa na Ukraine imezama.

Meli ya kivita ya Urusi MoskvaPicha: Russian Navy Black Sea Fleet/TASS/dpa/picture alliance

Ukraine imedai shambulizi lake dhidi ya meli ya Urusi katika  Bahari Nyeusi limeharibu vibaya meli hiyo lakini serikali ya Urusi ambayo awali ilisema meli hiyo iliyiokuwa ikitumika kurusha makombora katika eneo la pwani ya mashariki kuwa bado inaelea kama kawaida kwa sasa imezama.

Pasipo ufafanuzi wa kina Wizara ya Ulinzi imesema meli hiyo imezama baada ya kupata athari zilizotokana na moto.

Kwengineko, gavana wa eneo la Belgorod nchini Urusi anadai kijiji cha Spodaryushino, "kimeshambuliwa na  makombora" kutoka upande wa mpaka wa Ukraine, na kwamba kijiji hicho pamoja na kijiji cha jirani wakazi wake wamehamishwa kwa tahadhari. Hata hivyo taarifa hizo zimeshindikana kuthibitiswa.

Polisi ya Ufaransa yashiriki uchunguzi wa Mauwaji ya Bucha.

Polisi ya Ufaransa imepeleka ndege inayorushwa bila ya rubani katika anga ya eneo la Bucha, karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv ili kupiga picha kaburi la urefu wa mita 14 ambalo miili ya watu 70 iligundulika.

Timu ya wataalam 18 kutoka idara ya  polisi wa taifa hilo imekuwa ikifanya kazi kwa siku mbili kuchunguza na kubaini waliozikwa kwenye kaburi kubwa zaidi la watu wengi liliobainika hadi sasa katika mji huo ulioharibiwa vibaya kwa makombora ya Urusi.

Kwa kawaida timu hiyo inafanya kazi katika matukio ya kihalifu ya Ufaransa, majanga ya asili au ajali za barabarani. Kwa sasa ni sehemu ya operesheni kabambe ambayo inafanyika katika eneo hilo, ambalo liliwahi kudhibitiwa na majeshi ya Urusi, ambayo inaweza kusaidia katika kesi iliyopo katika mahakama ya uhalifu wa kivita ya mjini The Hague, Uholanzi.

Katika hatua hii, wachunguzi wanapiga picha za kawaida na video na kuchukua sampuli za vinasaba vya miili inayopatikana. Baada ya ugundulizi huo, inawezekana wataalamu wakiunganissha miili ya waliouwawa na jamaa zao. Vyote kwa pamoja vitakavyobainika vitasaidia katika uchunguzi wa ndani na wa kimataifa.

Machafuko katika eneo laBuchayamebeba dhana kubwa ya madai ya ukatili wa Urusi katika uvamizi wake nchini Ukraine. Wakazi katika eneo hilo waliwazika wenzao baada ya mzingiro wa Urusi, baada ya kujiondoa Machi 30, ikiwa ni baada ya kuukalia mji huo kwa takribani mwezi.