Watu 62 waangamia katika mripuko wa lori la mafuta Tanzania
10 Agosti 2019"Kulikuwa na mripuko mkubwa ambao mpaka sasa umewauwa watu 57," mkuu wa polisi wa mkoa huo Willbrod Mtafungwa akizungumza mapema leo na wanahabari.
Mashuhuda wameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kuwa waliona mabaki ya pikipiki kadhaa za bodaboda na miti iliyokuwa imeungua kutokana na nguvu za mlipuko huo.
Mtafungwa amesema waliouawa wengi wao ni wahudumu wa bodaboda na wakaazi wa eneo hilo waliofurika katika eneo la ajali kuchota mafuta baada ya lori hilo kuanguka. Polisi kisha wakasema baadaye kuwa moto huo umedhibitiwa.
Kamishna wa polisi wa mkoa wa Morogoro Stephen Kebwe amewaambia wanahabari katika eneo hilo la Msamvu, magharibi mwa Dar es Salaam kuwa eneo la Morogoro halijawahi kushuhudia mkasa wa kiwango hicho.
Alisema lori hilo lilipinduka kandoni mwa barabara na mafuta yakaanza kutiririka. "Tunawashirikisha madaktari wote wa hospitali ya Morogoro ili waliojeruhiwa watibiwe" aliongeza, bila kutoa idadi ya waliojeruhiwa.
Mikasa ya aina hiyo sio mipya barani Afrika.
Mwezi uliopitam watu 45 waliuawa na zaidi ya 100 wakajeruhiwa wakati lori la mafuta liliporipuka nchini Nigeria.
Mwezi Mei, tukio sawa na hilo lililotokea nchini Niger umbali mfupi tu kutoka uwanja wa ndege wa Niamey, na kuwauwa watu 80.
Miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya aina hiyo, watu 292 waliuwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Julai 2010, na Septemba 2015 karibu watu 203 waliuawa katika mji wa Maridi nchini Sudan Kusini