Watu 57 waokolewa kutoka boti za wahamiaji Lampedusa
6 Agosti 2023Walinzi wa Pwani ya Italia wamesema leo kuwa wamefanikiwa kuipata miili miwili ya wahamiaji na imewaokoa wengine 57 nje kidogo ya kisiwa cha Lampedusa. Taarifa hizo zimetolewa wakati karibu watu 30 wakiripotiwa kuwa hawajulikani waliko baada ya kutokea kwa ajali mbili za boti.
Soma pia: MFS: Ufaransa na Italia huwanyanyasa wahamia
Katika taarifa yao, walinzi hao wa pwani wameeleza kuwa miili ya watu wawili iliyopatikana ni ya mwanamke na mtoto wa umri wa mwaka mmoja kutoka Cote d'Ivoire.
Shirika la habari la ANSA limewanukuu watu walionusurika wakisema kuwa boti moja ilikuwa na watu 48, na ya pili ilibeba wahamiaji 42. Miili iliyopatikana na watu walionusurika walikutwa umbali wa kilometa 46 kusini mashariki mwa Lampedusa.
Soma pia: Wahamiaji zaidi ya 900 wafa maji pwani ya Tunisia
Kulingana na taarifa ya operesheni ya uokoaji kusini mwa kisiwa cha Lampedusa, boti za wahamiaji zilizozama zinaaminika kuwa zilikuwa zikitokea Sfax, mji ambao ni kitovu cha mzozo wa uhamiaji nchini Tunisia.