1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Watu 6 hatiani kwa mashambulizi ya kigaidi ya Brussels

26 Julai 2023

Mahakama ya Ubelgiji Jumanne imewatia hatiani watu 6 na wengine wawili kwa madai ya ugaidi, baada ya kesi kubwa zaidi nchini humo kuhusu mashambulizi ya bomu ya 2016 mjini Brussels yaliyosababisha vifo vya watu 32.

Belgien Brüssel | Prozessauftakt | Richterin Laurence Massart
Picha: Olivier Matthys/Pool/REUTERS

6 kati ya watu 10 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka wamepatikana na hatia ya mauaji na jaribio la mauaji kwa muktadha wa kigaidi, kwa ushiriki wao katika mashambulizi ya mabomu mawili yaliyolipuka katika uwanja wa ndege wa Brussels na bomu la tatu lililolipuka katika treni ya Metro nchini humo mnamo Machi 22 mwaka 2016.

Watu hao na wengine wawili pia wamepatikana na hatia pia ya kushiriki katika vitendo vya shirika la kigaidi. Wawili kati yao hawakupatikana na hatia. Vikao tofauti vya kuamua vifungo vyao vitafanyika mwezi Septemba.

Mawakili wakifuatilia kikao cha maamuzi katika kesi ya ugaidi mjini BrusselsPicha: Olivier Matthys/Pool/REUTERS

Mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya Paris akutwa na hatia

Miongoni mwa wale waliopatikana na hatia ni Salah Abdeslam, ambaye ndiye mshukiwa mkuu katika kesi kuhusu mashambulizi ya Paris yaliyosababisha vifo vya watu 130. Wakili wake Michel Bouchat alikuwa na haya ya kusema baada ya uamuzi huo kutolewa.

"Naweza kuwaambia kwamba nimevunjwa moyo sana sana na uamuzi uliotolewa na jopo la majaji. Na naongeza kwamba hatujaridhishwa kwa kweli na sababu zilizotolewa kwa uamuzi kufikiwa," alisema Bouchat.

Abdeslam aliyekuwa ametoroka Ufaransa, alikamatwa mjini Brussels siku nne kabla mashambulizi ya Ubelgiji kufanyika. Wengine waliopatikana na hatia ni Mohamed Abrini, aliyekwenda uwanja wa ndege wa Brussels na walipuaji wengine wawili wa kujitoa mhanga, ila akatoweka bila kulipua mkoba wake uliokuwa na vilipuzi. Mwengine alikuwa ni Osama Krayem ambaye ni raia wa Sweden aliyedaiwa kuwa mtu wa pili aliyepanga kufanya shambulizi katika usafiri wa treni mjini Brussels.

Majaji watoa uamuzi baada ya kuketi faragha wiki mbili

Oussama Atar anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo na anayedhaniwa kwamba aliuwawa nchini Syria, pia amepatikana na hatia katika kesi hiyo.

Washukiwa hao walisimama mbele ya zaidi ya watu 900, wakiwemo wahanga waliokuwa na majeraha ya kudumu ya kimwili na kisaikolojia, ndugu na jamaa za waliofariki na waokoaji wa kwanza waliofika maeneo ya matukio mara tu baada ya kufanyika mashambulizi hayo.

Washukiwa wakisiliza hukumu ya majaji mjini BrusselsPicha: Olivier Matthys/Pool/REUTERS

Uamuzi wa jopo la majaji 12 ulifikiwa baada ya kufanya kikao cha faragha cha wiki mbili, baada ya kuisikiliza kesi kwa kipindi cha miezi saba. Kesi hiyo ilikuwa inafanyika katika yaliyokuwa makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO, eneo lililotengwa mahsusi kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Vyanzo: Reuters/DPAE