1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Watu 6 wauawa kufuatia mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine

9 Machi 2023

Mashambulizi makubwa zaidi ya Urusi nchini Ukraine yamesababisha vifo vya watu 6 na kupelekea kukatika kwa umeme katika taifa hilo. Rais Zelenskiy amesema Moscow haitakwepa jukumu lake katika hilo.

Ukraine Krieg Kämpfe um Bachmut
Picha: Alex Babenko/REUTERS

Wanajeshi wa Ukraine walidungua karibu nusu ya makombora yaliyorushwa na Urusi katika takriban mikoa 10, wakati mapambano yakiendelea ili kuwania kuudhibiti mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine.

Mashambulizi mabaya  ya Urusi leo Alhamisi yalilenga eneo tulivu la Lviv magharibi mwa Ukraine na kuuacha mji wa pili wa Kharkiv bila nishati ya umeme wala huduma ya maji safi. Mashambulizi mengine yameripotiwa pia eneo la kusini magharibi la Odesa.  

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema adui amerejea katika mbinu zake mbaya na amerusha makombora 81 katika jaribio la kuwatisha raia wa Ukraine kwa mara nyingine. Hata hivyo Zelenskiy amesema wanaendelea na mapambano:

Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

"Nilifanya mkutano na jeshi na idara ya ujasusi. Mstari wa mbele wa vita, ulinzi wetu, vita vya Bakhmut na Donbas ndio kipaumbele chetu. Tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mbinu zetu zinachangia katika mkakati na mafanikio ya Ukraine katika vita hivi na kwenye maeneo yote yanayokaliwa kwa muda nchini mwetu."

Kwa miezi kadhaa Urusi imekuwa ikiishambulia kwa makombora na kwa kutumia ndege zisizo na rubani miundombinu muhimu nchini Ukraine, na hivyo kutatiza huduma za usambazaji wa umeme, maji na gesi kwa mamilioni ya watu.

  Soma pia:Bakhmut iko hatarini kuangukia mikononi mwa Urusi  

Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko Picha: DW

Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amesema watu wawili wamejeruhiwa huku asilimia 15 ya kaya zikiwa hazina umeme na asilimia 40 zikishindwa kupasha joto majumba yao kufuatia milipuko katika maeneo mawili ya mji mkuu wa Ukraine.

Gavana wa mkoa wa Lviv magharibi mwa Ukraine amesema miili ya watu watano imepatikana kwenye vifusi baada ya nyumba yao kushambuliwa kwa kombora, huku gavana wa eneo la mashariki la Dnipropetrovsk akisema kuwa mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 34 ameuawa.

Shirika la nishati ya nyuklia la Ukraine limesema mashambulizi hayo pia yamesitisha usambazaji wa umeme kwenye kinu cha nyuklia kikubwa zaidi barani Ulaya cha Zaporizhzhia, ambacho kinadhibitiwa na majeshi ya Urusi. Kwa mara ya sita tangu kinu hicho kidhibitiwe na vikosi vya Urusi, sasa kinafanya kazi kwa kutumia jenereta za dizeli ambazo zina uwezo wa kumudu kwa siku 10 pekee.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Zelenskiy amesema wavamizi wanaweza tu kuwatishia raia. Ni hayo tu wanayoweza kuyafanya. Lakini hilo halitowasaidia. Hawatakwepa jukumu lao katika jambo walilolifanya.

(rtre, afpe)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW