1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maporomoko yauwa 65 na kujeruhi 116 Tanzania

Deo Kaji Makomba
5 Desemba 2023

Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya tope kutoka katika mlima Hanang uliopo mkoani Manyara imeongezeka na kufikia 65 na majeruhi 116.

Tansania | Tote nach Erdrutsch in Hanang
Picha: Tanzania’s Ministry of Interior

Taarifa hizo zinatolewa wakati  kazi ya uokoaji ikiendelea katika maeneo ya Kateshi na kijiji cha Gendabi. Idadi ya vifo hivyo huenda ikaongezeka kutokana na hali ilivyo katika maeneo yalioathirika kutokana na maporomoko hayo. 

Akizungumza na wananchi katika mji wa Kateshi ambao umekumbwa na maporoko ya tope kutoka katika mlima Hanang, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa zoezi la uokoaji bado linaendelea na kwamba juhudi zinafanyika ili kuweza kufungua miundombinu iliyoharibiwa vibaya na maporomoko hayo.

Juhudi za vikosi vya ulinzi na usalama

Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaliwa alipowatembela majeruhi katika hospitali ya Manyara.Picha: Ministry of Health of Tanzania

Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Tanzania vilivyoweka kambi wilayani Hanang, vinaendelea na zoezi la uokozi huku wananchi nao wakionekana kuendelea kuokoa vitu mbalimbali katika nyumba zao na wengine katika sehemu zao za biashara.

Maporomoko hayo yamegharimu maisha ya watu huku wengine wakikosa mahali pa kuishi baada ya makazi yao kusombwa na maporomoko ya tope na hivyo kuhifadhiwa katika kambi maalumu kwa ajili ya kupata misaada ya kiutu. DW imetembelea katika shule ya sekondari ya Katesh  ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahifadhi waathiriwa wa maporoko hayo. Bi. Christina Michael ni miongoni wa waathirika aliyepoteza mtoto wake wakati wa maporomoko hayo.

Soma zaidi:Idadi ya waliokufa kufuatia maporomoko ya ardhi Tanzania yafikia 68

Mafuriko hayo yaliyoleta maafa na athari kubwa ikiwemo nyumba 28 kusombwa na maporomoko. Mafuriko mabaya zaidi yaliosababisha na mvua za El Nino yameyakumba mataifa ya Afrika mashariki na kusababisha mamia ya watu kuyahama makaazi yao ikiwemo Tanzania,Kenya,Somalia na hata Ethiopia.

Mafuriko hayo yanatokea baada ya ukame mbaya kulikumba eneo la Pembe ya Afrika katika kipindi cha miaka 40.

DW Manyara

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW