Watu 70 wauwawa Syria
1 Julai 2016Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu limesema wanajeshi 30 na wapiganaji waasi 39 wameuwawa katika mapigano yaliotokea katika maeneo ya Al-Maleh, kaskazini mwa Aleppo tangu jioni ya Alhamisi. Wapiganaji wa kundi la Al-Nusra, linalotajwa kuwa tawi la al-Qaeda nchini Syria vilevile ni miongoni mwa waliuwawa.
Serikali ya Rais Bashar al Assad imekuwa katika jaribio la kutaka kulidhibiti eneo la Al-Maleh kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Jeshi lake kwa miezi kadhaa limekuwa likijaribu kuuzingira mji wa Aleppo kwa kuzuia hudumua katika ya wilaya zinazodhibitwa na waasi katika mji huo na karibu na Uturuki, ambayo inaunga mkono wapiganaji waasi.
Jitihada za Urusi
Karibu wiki sasa majeshi ya utawala wa Syria, yakiungwa mkono na ndege za kivita za Urusi yamekuwa yakipambana vikali kuudhibiti mji wa Al-Maleh. Utawala wa Assad vilevile upo katika jitihada ya kuivuruga barabra muhimu ya Castello, inayotokea mpakani mwa Uturuki kuelekea vitongoji ambavyo vinakaliwa na waasi vya Aleppo.
Tovuti inayoegemea upande wa utawala Al-Masdar imeripoti kuwa jeshi la Syria limejiondoa katika maeneo ya mashambani la Al-Maleh wakati wakikabiliana na mashambilizi makali yanayoongozwa na wapiganaji wa Kundi la Al-Nusra Front. Ripoti hiyo inasema waasi waliyashambulia majeshi ya serikali kwa mabomu mawili ya kujitoa muhanga.
Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini humo limesema watoto wawili ni miongoni mwa waliuwawa kwa bomu katika eneo linalodhibitiwa na waasi mjini Aleppo. Idadi kubwa ya maeneo ya jimbo la Aleppo yanadhibitiwa na Al-Nusra Front na washirikia wao makundi ya wenye itikadi kali za dini ya Kiislamu.
Lakini mkoa huo uliyokuwa mji mkuu wa kibiashara kabla ya vita, umegawanyika tangu Julai 2012. Kuna maeneo ya waasi na mengine yanadhibitiwa na serikali.
Katika hatua nyingine shirika hilo la uangalizi vilevile jana liliripoti jana kuwa watu kumi na watatu, wakiwemo watoto wanne vilevile wameuwawa kwa makombora katika mkoa wa Ghouta Mashariki uliyoko karibu na Damascus. Mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa miaka mitano umesababisha vifo vya zaidi ya watu 280,000.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga