1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 73 wafariki baada ya boti kuzama kwenye pwani ya Syria

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
23 Septemba 2022

Watu wasiopungua 73 wamekufa baada ya boti iliyowabeba wahamiaji kutoka Lebanon kuzama nje ya pwani ya Syria katika ajali mbaya zaidi ya boti kutoka Lebanon katika miaka ya hivi karibuni.

Syrien | Rettungsaktion am Hafen von Tartous
Picha: Saleh Sliman via REUTERS

Mamlaka ya Syria imesema baadhi ya wanafamilia wa wahasiriwa wameanza kuvuka na kuingia nchini Syria kutoka nchi jirani ya Lebanon ili kuja kushiriki kwenye zoezi la kuitambua miili ya wapendwa wao na pia kufanya mchakato wa kuirejesha nyumbani miili hiyo. Waziri wa Afya wa Syria Mohammed Hassan Ghabbash amesema watu 20 wameokolewa na wanapokea matibabu katika hospitali ya al-Basel iliyo katika mji wa pwani wa Syria wa Tartus.

Ambulensi zikisubiri waathiriwa katika ajali ya boti iliyotoka Lebabnon katika mji wa Tartus nchini Syria.Picha: Saleh Sliman via REUTERS

Mkasa huo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea unaohusisha mamia ya raia wa Walebanon, Wasyria, na Wapalestina wanaojaribu kukimbia mzozo uliolikumba taifa la Lebanon kupitia baharini kuelekea bara Ulaya.

Nchini Lebanon maelfu ya watu wanakabiliwa na hali ngumu mno na wengi pia wamepoteza kazi zao na wakati huo huo sarafu ya pauni ya Lebanon imeshuka thamani yake kwa zaidi ya asilimia 90 hali inayosababisha dhiki kwa familia na kuzitumbukiza kwenye lindi la umasikini wakati ambapo wanashindwa kununua bidhaa nyingi kutokana na bei za vitu kupanda mno. Lebanon ina wakazi milioni 6, ikiwa ni pamoja na watu milioni 1 ambao ni wakimbizi kutoka Syria na imekuwa ikikabiliwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi tangu mwishoni mwa mwaka wa 2019.

Bidhaa zimepanda bei mno nchini Lebanon huku thamani ya pauni ya Lebanon ikianguka kwa asilimia 90.Picha: Aziz Taher/REUTERS

Afisa mmoja wa bandari ya Syria ameliambia shirika la habari la serikali, SANA, kuwa miili 31 ilielea hadi ufukweni na iliyosalia iliopolewa na wafanyakazi wa pwani ambao wamekuwa wakifanya shughuli ya kuwatafuta walioathirika kuanzia siku ya Alhamisi jioni.

Maelfu ya Walebanon, Wasyria na Wapalestina wamekuwa wakiondoka kutoka nchini Lebanon kwa kutumia boti katika miezi iliyopita kwa lengo la kwenda kutafuta fursa bora zaidi katika bara Ulaya.

Wakimbizi kwenye boti wakifanya safari za hatari kwatika bahari ya MediterraniaPicha: Joan Mateu/AP/picture alliance

Mwaka jana Lebanon ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaotumia ufuo wake kujaribu kuvuka kwa boti zilizojaa watu wakijaribu kuelekeka bara Ulaya. Makumi ya watu walizama mnamo mwezi Aprili, wakati boti iliyojaa watu ilipokimbizwa na jeshi la wanamaji la Lebanon kwenye pwani ya Tripoli, kaskazini ya nchi hiyo.

Vyanzo:AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW