1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 75 wauawa nchini Iraq

Kabogo Grace Patricia19 Agosti 2009

Watu hao wameuawa kufuatia mfululizo wa mashambulio ya mabomu yaliyotokea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Wananchi wa Iraq wakiangalia gari lililoripuliwa na bomu katikati ya Baghdad, Iraq.Picha: AP

Watu 75 wameuawa katika mfululizo wa mashambulio ya mabomu kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad, yakiwa ni mashambulio mabaya kutokea tangu majeshi ya Marekani yaondoke kwenye miji ya nchi hiyo. Katika mashambulio hayo kiasi watu wengine 400 wamejeruhiwa.

Mashambulio hayo yaliyotokea nje ya ofisi za wizara za serikali ya Iraq yameingiliana na kumbukumbu ya miaka sita tangu kutokea kwa shambulio la bomu katika eneo la Umoja wa Mataifa mjini Baghdad na kumuua mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, Sergio Vieira de Mello na watu wengine 21.

Lori moja liliripuka nje ya ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq katika makaazi ya watu, karibu na eneo lenye ulinzi mkali la Green Zone. Shambulio hilo la bomu limeharibu pia matenki ya maji katika nyumba karibu na wizara hiyo na kusababisha maji kutiririka hovyo kwenye nyumba hizo.

Lori jingine liliripuka nje ya Wizara ya Fedha iliyopo kaskazini mwa Baghdad katika eneo la Waziriyah, na kuharibu daraja karibu na eneo la wizara na kusababisha watu 200 kujeruhiwa. Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi, wamesema watu 47 waliuawa katika shambulio lililotokea kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, huku shambulio la Wizara ya Fedha likiwa limewaua watu 28.

Msemaji wa Jeshi la Iraq, Meja Jenerali, Qassim Atta amesema wanakishutumu chama cha Baathist kwa kuhusika na mashambulio hayo ya kigaidi. Meja Jenerali Atta, amesema vikosi vya usalama vimewakamata viongozi wawili wa juu wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika eneo la karibu la Mansur lililopo magharibi mwa Baghdad.

Afisa wa Wizara ya Ulinzi, amesema bomu la kutegwa kwenye gari liliripuka pia katika soko kwenye eneo la Bayaa na kuwaua watu wawili na wengine watano wamejeruhiwa. Aidha, amesema mabomu mawili yaliripuka ndani ya eneo lenye ulinzi mkali la Green Zone, ambako kuna ofisi za balozi za kigeni na ofisi za serikali na jingine moja liliripuka nje ya eneo hilo.

Mashambulio hayo ya mabomu yametokea siku chache kabla Waislamu hawajaanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan baadaye wiki hii. Mashambulio ya leo yamesababisha vifo vingi tangu kutokea kwa mashambulio ya Februari Mosi, mwaka 2008, ambapo mabomu yaliripua masoko ya Baghdad na kuwaua watu 98.

Japokuwa mizozo imepungua mjini Baghdad katika miezi ya hivi karibuni, mashambulio dhidi ya vikosi vya usalama na raia bado yanaendelea mjini humo, pamoja na kwenye mji wa Mosul na Kirkuk. Idadi ya watu waliouawa katika mashambuio nchini Iraq imepungua kutoka 437 mwezi Juni hadi 275 mwezi uliopita, kufuatia kuondoka kwa majeshi ya Marekani kwenye miji ya nchi hiyo, Juni 30, mwaka huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW