1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya,Tanzania na Burundi zakumbwa na mafuriko mabaya zaidi

28 Aprili 2024

Mvua za Masika zinazoendelea kunyesha katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki zasababisha vifo na adha kubwa huku Kenya ikitahadharisha mvua kubwa zaidi itanyesha ndani ya saa 24 zijazo

BdTD | Kenia | Überschwemmungen in Nairobi
Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Watu 76 wamepoteza maisha nchini Kenya kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za masika zilizoanza kunyesha tangu mwezi Machi. Serikali nchini humo imetoa tahadhari kwa wananchi kujiandaa  kwa mvua kubwa zaidi.

Mafuriko yasababisha adha kwa wananchi KenyaPicha: REUTERS

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura alisema, barabara na vitongoji vimefurika maji na zaidi ya watu 13,000 wameyahama makaazi yao katika jumla ya kaya 24,000. Ameongeza kuwa mji mkuu wa Nairobi ndio umeathirika zaidi huku idadi ya watu 32 wakifariki na zaidi ya 16,000 kuyahama makaazi.

Akitowa maelezo Jumamosi kuhusu hali ilivyo alisema watu wengine sita walipoteza maisha ndani ya kipindi cha saa 12 hivyo kuifanya idadi jumla ya waliokufa hadi jumamosi kufikia 76 huku wengine 29 wakijeruhiwa na 19 wakiwa bado hawajulikani walipo. 

Mabwawa yote matano  yanayojumuisha maeneo ya mradi wa uzalishaji umeme wa Seven Forks kwenye eneo la mto Tana, imefurika kabisa. Serikali inasema huenda maji ya mabwawa hayo yakafurika zaidi  ndani ya kipindi cha saa 24 na kwahivyo wakaazi wa maeneo yanayopakana na mabwawa hayo wameshauriwa kwenda kwenye maeneo ya nyanda za juu.

Mafuriko mtaa wa Mathare-NairobiPicha: Daniel Irungu/EPA

Mvua katika Nchi jirani

Mvua za masika zimesababisha adha kubwa pia katika nchi jirani ya Tanzania ambako takriban watu 155 wameshapoteza maisha kufuatia mafuriko na maporomoko ya udongo.

Mkaazi mmoja wa mtaa unaoitwa Jangwani ulioko katika jiji la Daresalam,aliyejitambulisha kwa jina la Khatibu Kipara ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali inatisha sana katika eneo hilo.

Mkaazi huyo mwenye umri wa miaka 35, amesema watu wengi wameathiriwa na mafuriko akiwemo yeye mwenyewe na wengi wamepoteza mali zao,makaazi yao yakiwa yamefurika maji.Soma pia:Idadi ya vifo kutokana na mafuriko Kenya yapanda hadi 120

Nchini Burundi,ambayo ni moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, takriban watu 96,000 wameachwa bila makaazi kutokana na mvua za mfululizo zilizoanza miezi kadhaa iliyopita kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa na serikali ya nchi hiyo.

Uganda nako kumeshuhudiwa vimbunga vikali vilivyosababisha mito kufurika na kuvunja kingo ambapo vifo vya watu wawili vimethibitishwa na watu chungunzima wakiachwa bila makaazi katika maeneo ya vijijini.

Magari yakwama kufuatia mafuriko KenyaPicha: Andrew Wasike/DW

Zaidi ya watu 300 walipoteza maisha mwaka jana 2023 kufuatia mvua na mafuriko yaliyoshuhudiwa katika nchi za Kenya,Somalia na Ethiopia,  wakati  kanda hiyo ya Afrika mashariki ilipokuwa ikijaribu kujikwamua kutokana na ukame mbaya kabisa ambao haujawahi kutokea kwa kipindi cha miongo minne na uliosababisha mamilioni ya watu kukosa chakula

Hali ya hewa ya El Nino ni  mabadiliko ya kiasili ya kimazingira yanayofungamanishwa na ongezeko la joto duniani inayosababisha katika baadhi ya maeneo ukame na mvua kubwa kwenye maeneo mengine ya ulimwengu. Shirika la masuala ya hali ya hewa la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Machi lilisema kwamba hali ya hewa ya El Nino inayoshuhudiwa sasa ni moja ya zile mbaya kabisa kati ya tano zilizowahi kurekodiwa katika historia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW