1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya anga ya Israel yawauwa watu 87 Gaza

Angela Mdungu
20 Oktoba 2024

Takriban Wapalestina 87 wameuwawa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye mji wa Bet Lahia ulio kaskazini mwa Gaza kama ilivyoripotiwa na shirika la ulinzi wa raia la Gaza.

Wakazi wa Al-Maghazi, Ukanda wa Gaza, baada ya shambulio la anga la Israel
Baadhi ya Wapalestina wakiendelea na shughuli ya uokoaji baada ya mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Omar Ashtawy/APA Images/Zumapress/picture alliance

Ofisi ya habari ya mamlaka katika Ukanda wa Gaza iliyo chini ya Hamas imethibitisha vifo hivyo, ikiongeza kuwa miongoni mwao ni wanawake na watoto, huku watu wengine wakiwa bado wamekwama chini ya vifusi vya majengo yaliyobomoka. Israel imesema kuwa ililenga kundi la Hamas, lakini imetilia shaka idadi ya vifo vilivyoripotiwa.

Soma zaidi: Zaidi ya watu 400 wauawa Gaza ndani ya muda wa wiki mbili

Wakati huo huo, shirika la habari la Lebanon limesema kuwa Israel imefanya mashambulizi dhidi ya vijiji na miji 50 kusini mwa Lebanon, likiwemo jiji la Nabatiyeh, ambalo limekumbwa na mashambulizi makali, na waokoaji bado wanatafuta watu waliofunikwa na vifusi. Israel pia inasema imefanya mashambulizi dhidi ya makao makuu ya ujasusi na kiwanda cha silaha cha Hezbollah mjini Beirut.