1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu asilimia 40 Afrika ya Kusini hawana ajira

Epiphania Buzizi27 Juni 2005

Chama kikuu cha wafanyakazi nchini Afrika ya Kusini kimeitisha mgomo wa kazi kupinga ongezeko la ukosefu wa ajira

Maafisa wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini Afrika ya Kusini COSATU,wamesema kwamba wafanyakazi wengi bado wanalipwa mishahara midogo, na kufanyakazi ya ujira mdogo kama ilivyokuwa enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kinafikia asilimia 25, wakati ambapo chama cha wafanyakazi nchini Afrika ya Kusini cha COSATU, kinasema kwamba idadi halisi ya watu wasio na ajira nchini humo inafikia asilimia 40.

Chama hicho kikuu cha wafanyakazi nchini Afrika ya Kusini,COSATU,kinasema kuwa mgomo huo wa siku moja ambao vyama vya wafanyakazi vinatarajiwa kuwa utasababisha shughuli kuzorota katika miji mbali mbali nchini humo,utafuatiwa na mgomo mwingine ikiwa serikali ya Afrika ya Kusini pamoja na viwanda hawatachukua hatua yoyote kutekeleza matakwa ya wafanyakazi hao.

Msemaji wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini humo Patrick Craven, amebainisha kuwa hawawezi kusema kwamba uchumi wa nchi hiyo unakua sana, wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na talizo la watu wasio na ajira kwa asilimia 40. Msemaji huyo wa COSATU, ameeleza kuwa wafanyakazi wanataka kuona kwamba kazi zinaongezeka badala ya kuzipunguza.

Kwa upande mwingine, msemaji wa kampuni ya madini ya AngloGold Ashanti amesema kwamba wafanyakazi wengi wa kampuni hiyo leo hawakuhudhuria kazini, lakini hakusema ni kwa kiwango gani hatua hiyo itaathiri uzalishaji.

Chama cha COSATU ambacho ni shirikisho la jumuiya za wafanyakazi,na ambacho ni mshirika wa karibu wa chama tawala cha ANC, kimesema kuwa kinatarajia idadi kubwa ya wafanyakazi kutoka sekta ya madini kushiriki kwenye mgomo huo wa kazi.

Maelfu ya wafanyakazi katika migodi ya dhahabu walipoteza kazi miaka michache iliyopita, kutokana na kupanda kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo Rand.

Lakini mkuu wa operesheni za uchimbaji wa dhahabu nchini Afrika ya Kusini, katika kampuni ambayo ni ya nne kwa ukubwa Duniani kwa kuzalisha dhahabu, Mike Prinsloo, amesema kwamba ni wafanyakazi 15 elfu pekee kati ya elfu arubaini wa kampuni hiyo ambao hawakuweza kufika kazini.

Katika kitongoji cha Soweto, Kusini Magharibi mwa mji wa kibiashara Johannesburug, safari za gari moshi zimeripotiwa kupungua ikilinganishwa na utaratibu wa kawaida, ambapo wasafiri wengi wamearifiawa kujerea majumbani mwao.

Wakati huo huo, msemaji wa chama kikuu cha wafanyakazi nchi ni Afrika ya Kusini, Patrick Craven, amebainisha kuwa ni mapema mno kueleza namna mgomo wa wafanyakazi ulivyofanikiwa,lakini ameongeza kusema kuwa umati wa watu tayari ulikuwa umekusanyika katika mitaa.Amefafanua zaidi kuwa wafanyakazi wengi watafika kazini na kuacha tu ujumbe kueleza msimamo wao kuhusu mgomo huo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW