Watu kadhaa wajeruhiwa kwenye mlipuko jijini London
15 Septemba 2017Polisi nchini Uingereza wanalichukulia tukio hilo kuwa ni kitendo cha ugaidi baada mlipuko wa bomu kutokea katika eneo ambalo lilikuwa lina msongamano wa watu. Kamishna Mark Rowley mkuu wa kupambana na ugaidi amesema wengi kati ya watu waliojeruhiwa walipata majeraha yanayotokana na kuungua kwa moto huku wengine wakiwa wameumizwa baada ya kutokea mtafaruku huo uliosababisha watu kukanyagana. Kamishna Rowley amesema maafisa wa polisi bado wanaangalia picha za CCTV ili kubaini kilichotokea katika tukio hilo. Taarifa zaidi kutoka duru za hospitali zinasema kuwa watu waliojeruhiwa hawamo katika hali mahututi.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May baada ya kuongoza kikao cha dharura cha usalama kinachoitwa COBRA amesema kiwango cha tishio la kigaidi nchini Uingereza bado ni cha juu ikiwa na maana kwamba uwezekano wa kushambuliwa tena nchi hiyo upo hata hivyo tukio hilo halikusabaisha kiwango hicho kuongezeka na kuwa cha hali ya hali ya hatari. Waziri mkuu May aliongoza kikao hicho ambacho kiliwajumuisha maafisa wa serikali na wenzao wa masuala ya usalama. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema ni jambo zuri kutafakari kwanza kabla ya kutamka maneno. Johnson amewaomba watu wote wawe watulivu na kujaribu kuendelea na shughuli zao kama kawaida wakati ambapo polisi wa kitengo kinachohusika na usalama katika mfumo wa usafiri wa jiji la London wakiendelea kufanya uchunguzi na kisha watatoa taarifa zaidi kwenye mtandao wao.
Shirika la ujasusi la nchini Uingereza M15 linasaidiana na wapelelezi pamoja na polisi na limesema huenda udhibiti zaidi wa hali ya usalama ukaongezeka jijini London mwishoni mwa wiki hii. Tukio hilo la kigaidi ni la tano kutokea katika kipin di cha miezi sita nchuni Uingereza kutokea mwezi machi pale mtu mmoja alipo liendesha gari lake mahala ambapo watu walikuwa wanapita na baadae akashuka kwenye gari hiyo na kumshambulia polisi mmoja kwa kisu nje ya bunge la Uingereza. Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa wamelaani shambulio hilo. Rais wa Marekani Donald Trump amesema watu wanaofanya vitendo hivyo ni wagonjwa wa akili na kwamba polisi ni lazima izidishe doria.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/DPAE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman