Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi mjini Hamburg
9 Machi 2023Kwa mujibu wa ripoti kadha za vyombo vya habari, shambulio hilo limetokea katika kanisa la Mashahidi wa Jehova katika mtaa wa Deelboege katika wilaya ya Grossborstel mjini Hamburg.
Polisi mjini Hamburg katika taarifa yake wamesema kuwa "watu wote waliofariki walikuwa na majeraha ya risasi".
Kituo cha utangazaji cha NDR kimemnukuu msemaji wa polisi aliyesema kwamba mkasa huo umetokea majira ya saa tatu usiku ambapo mshambuliaji au washambuliaji wasiojulikana waliwafyatulia watu risasi kanisani. Wakaazi wa eneo hilo wameamuriwa kubaki ndani na kuepuka eneo hilo, polisi walisema, na kuongeza kuwa mitaa inayozunguka kanisa imezingirwa.
Msemaji wa polisi katika eneo la tukio amesema kuwa simu za kwanza za dharura zilipigwa karibu saa tatu na robo baada ya milio ya risasi kusikika katika jengo la kanisa. Kupitia Twitter polisi wamesema kuwa "watu kadhaa wamejeruhiwa vibaya, wengine hata kufa" katika tukio hilo.
Kengele ya "tahadhari kubwa" katika eneo hilo ilikuwa imepigwa kwa kutumia programu ya kwenye simu na polisi waliwataka wakaazi kusalia majumbani.
Polisi hawakutoa idadi kamili ya waliouawa, lakini vyombo vya habari kadhaa vya taifa vya Ujerumani vilisema watu wasiopungua sita waliuawa.
Kulingana na polisi, bado haijawa wazi nini kimesababisha mkasa huo. "Hadi sasa, hakuna taarifa zilizothibitishwa juu ya nini kimechangia uhalifu", imesema taarifa ya polisi kupitia Twitter. "Tunawaomba msisambaze taarifa ambazo hazijathibitishwa au uvumi".
HABARI ZAIDI ZITAKUJIA.......