1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Watu kadhaa wauawa katika shambulizi jipya nchini Ukraine

7 Aprili 2023

Watu kadhaa wameuawa kwenye shambulizi jipya katika mji wa Donetsk unaothibitiwa na Urusi Mashariki mwa Ukraine, ijapokuwa kufikia Alhamisi (6.04.2023) idadi kamili haikuwa imethibitishwa.

Ukraine-Krieg | Ukrainische Soldaten an der Front bei Bachmut
Picha: Libkos/AP Photo/picture alliance

Baadhi ya ripoti za Urusi zinasema watu wanne wameuawa huku nyingine zikitaja kuuawa kwa watu tisa. Kulingana na ripoti za Urusi, shambulizi hilo lililolenga msafara wa magari lilifanywa kwa kutumia makombora ya Marekani aina ya Himars. Video zilionesha magari yalioharibika pamoja na miili kadhaa ya waliokufa. Hata hivyo ripoti hizo hazikuweza kudhibitishwa kwa njia huru.

Mapigano bado yaendelea Bakhmut

Urusi imeteka rasmi eneo la Donetsk lakini bado inathibiti tu kiasi kidogo zaidi ya nusu ya jimbo hilo . Wakati huo huo mapigano makali yanaendelea katika eneo la Bakhmut lililoko katika jimbo la Donetsk ambapo vikosi vya Ukraine vinaendelea kupinga majaribio ya Urusi ya kuuteka mji huo ambao ulikuwa makazi ya watu 70,000.

Mkuu wa wagner asema Urusi yahitaji wiki nne kuiteka Bakhmut

Kulingana na ujumbe aliotuma kwa njia ya telegram, Yevgeny Prigozhin, mkuu wa kundi la mamluki la Urusi la Wagner, amesema huenda ikaichukuwa Urusi wiki tatu hadi nne kuuteka mji wa Bakhmut. Matamshi yake yanakuja siku kadhaa baada ya kudai kuwa mji huo tayari umetekwa. Prigozhin pia amesema Urusi bado inatafuta kukata laini za usambazaji za wanajeshi wa Ukraine, hatua itakayoiwezesha kuingia mji huo kutoka pande tofauti na kuendelea na uharibifu wa maeneo muhimu ya kijeshi.

Yevgeny Prigozhin - Mkuu wa kundi la mamluki la Urusi la WagnerPicha: AP Photo/picture alliance

Prigozhin alikuwa akizungumza katika eneo la makaburi la wanachama wa kundi lake na kusema kuwa eneo hilo linapaswa kuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo akiongeza kuwa wapiganaji wake wamepata hasara kubwa katika kuipigania Bakhmut katika muda wa wiki chache zilizopita.

Vikosi vya Ukraine vyathibiti eneo la Magharibi mwa Bakhmut

Wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakiutetea mji wa Bakhmut kwa miezi kadhaa, lakini maeneo mengi ya mji huo na sehemu za katikati tayari ziko chini ya udhibiti wa Urusi. Hata hivyo, vikosi vya Ukraine vimedhibiti sehemu ya magharibi ya mji huo.

Vikosi vya Ukraine vyapanga mashambulizi ya msimu wa machipuko

Kwa ukakamvu zaidi, vikosi vya Kiev vinaandaa mashambulizi ya msimu wa machipuko kukomboa maeneo yanayothibitiwa na vikosi vya Urusi ijapokuwa hakuna habari nyingi kuhusu hatua hiyo, huku watu wachache tu wakifahamu eneo na wakati wa mashambulizi yaliyopangwa.

Baadhi ya watu wanatarajia wanajeshi wa Ukraine kuweka shinikizo katika mji wa Pwani wa Melitopol hatua itakayovigawanya vikosi vya Urusi. Hata hivyo, jeshi la Urusi limepanua pakubwa maeneo yake ya ulinzi katika miezi ya hivi karibuni kuzuia shambulizi hilo linalotarajiwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW